Arsenal wanalo hilo Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Miamba hiyo ya Emirates imefuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya 16 bora baada ya kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Liverpool na Barcelona kwenye msimamo wa League Phase ya michuano hiyo.
LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Arsenal inakabiliwa na njia ngumu katika mchakamchaka wao wa kufukuzia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu baada ya droo ya mchujo.
Miamba hiyo ya Emirates imefuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya 16 bora baada ya kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Liverpool na Barcelona kwenye msimamo wa League Phase ya michuano hiyo.
Lakini, sasa inaweza kukabiliana na ratiba ngumu kwenye 16 bora, ikielezwa inaweza kupangwa na Juventus endapo kama miamba hiyo ya Italia itafanikiwa kuisukuma nje Lille ya Ufaransa kwenye mechi mbili za mchujo za nyumbani na ugenini.
Kama si Juventus, basi Arsenal inaweza kukabiliana na mshindi kati ya Feyenoord na AC Milan kwenye hatua hiyo ya raundi ya 16 bora.
Kama itapenya kwenye hatua hiyo, balaa zaidi linawasubiri kwenye robo fainali. Kinachoonekana ni kwamba Arsenal inaweza kupangwa na kucheza na moja ya timu hizi, Manchester City, Real Madrid na Bayern Munich. Na kama si vigogo hao, basi inaweza kupangwa kucheza na Bayer Leverkusen, Atletico Madrid au Celtic.
Liverpool, Paris St Germain au Barcelona zinaweza kuja kwenye hatua ya nusu fainali, jambo linaloonyesha Arsenal ilivyo na njia ngumu ya kufikia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ambayo itapigwa huko Munich, Ujerumani.
Man City nayo imeonekana kuwa na njia ngumu, ikiwamo ya hatua ya mchujo, ambapo watakabiliana na mabingwa mara 15, Real Madrid. Lakini, Liverpool inaonekana kuwa na ratiba nyepesi kidogo hadi hapo itakapofika nusu fainali, ambapo inaweza kupangwa kucheza na PSG na Borussia Dortmund.
Aston Villa ipo kwenye njia nyepesi kama ilivyo kwa Liverpool, ambapo inaweza kupangwa kucheza na Club Brugge, Atalanta, Sporting au Dortmund kwenye raundi ya 16 bora.