Arsenal waambiwa kitu kuhusu Isak
Muktasari:
- Isak, 25, amekuwa kwenye kiwango bora sana kwa sasa, akifunga mabao 10 katika mechi tisa za mwisho, ikiwamo moja alilofunga dhidi ya Arsenal kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Ligi.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeambiwa kwamba itawagharimu zaidi ya Pauni 115 milioni kumsajili staa wa Newcastle United, Alexander Isak - uhamisho utakaoweka rekodi kweye soka la England na ndiyo maana itakuwa ngumu kwao kukamilisha dili hilo.
Isak, 25, amekuwa kwenye kiwango bora sana kwa sasa, akifunga mabao 10 katika mechi tisa za mwisho, ikiwamo moja alilofunga dhidi ya Arsenal kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Ligi.
Hatima ya straika Isak ipo kwenye shaka kubwa kwelikweli kwa sasa huko Newcastle ikitokana na timu nyingi kuhitaji huduma yake ikiwamo Arsenal.
Newcastle bado inataka kuweka sawa vitabu vyake vya kihesabu, hivyo itakuwa tayari kufanya biashara kama kutakuwa na ofa ya maana kwa fowadi huyo.
Lakini, mabosi wa St James’ Park wanafichua kwamba staa huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Real Sociedad bei yake anayouzwa ni zaidi ya Pauni 115 milioni, kiwango ambacho Chelsea ilitumia kulipa kunasa saini ya kiungo Moises Caicedo mwaka 2023.
Isak bado ana mkataba wa miaka mitatu na nusu kwenye kikosi cha Newcastle na sasa anachopambana ni kuisaidia timu hiyo kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa imeshinda kwenye mechi saba mfululizo.
Arsenal kwa sasa haina pesa za kutosha, hivyo imefungua milango ya kupokea ofa ya kumpiga bei Gabriel Jesus kwenye dirisha la majira ya kiangazi, huku ikiamini ataachana pia na Thomas Partey, ambaye mshahara wake wa Pauni 150,000 kwa wiki ukiondoka kwenye bili yao itawaweka sawa.
Kwa ujumla, straika Isak amefunga mabao 13 kwenye mechi 20 alizocheza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kuwekwa kwenye rada za vigogo wengi Ulaya.