Arsenal vs Spurs... Gemu lenye ufundi mwingi
Muktasari:
- Arsenal itakuwa nyumbani uwanjani Emirates kuwakabili mahasimu wake wakubwa, Tottenham Hotspur katika mechi ya kibabe kabisa kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: LIGI imerudi na gumzo la wikiendi ni kipute cha North London Derby.
Arsenal itakuwa nyumbani uwanjani Emirates kuwakabili mahasimu wake wakubwa, Tottenham Hotspur katika mechi ya kibabe kabisa kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England.
Mechi hiyo itakayochezwa Jumapili, timu zote zitakosa huduma za mastaa kadhaa huku Arsenal ikibainisha haitakuwa na beki wake wa kati, Gabriel wakati straika Viktor Gyokeres akiwa kwenye hatihati kubwa ya kucheza mechi yake ya kwanza ya North London derby.
Lakini, kocha Mikel Arteta ana wigo mkubwa wa machaguo kwenye kikosi chake na huenda akashuka uwanjani na mbinu ambazo Spurs itashindwa kukabiliana nayo.
Kipute hicho cha Arsenal na Spurs kitaamriwa kwa mambo ya kiufundi. Arsenal itatumiaje udhaifu wa Spurs na mahasimu hao watajibu vipi kuonyeshana ubabe katika mechi hiyo?
UJANJA WA ARSENAL
Mabeki wa Spurs, Cristian Romero na Micky van de Ven watakuwa kwenye hatari ya kutumiwa na Arsenal kwenye mbinu zao kwa maana ya kuwafanya waondoke kwenye maneo yao, hivyo kuwaruhusu Declan Rice na Eberechi Eze kuingia kwenye penalti boksi.
Moja ya kitu kikubwa kuhusu Spurs mabeki wake wamekuwa na kawaida ya kuwakimbiza wachezaji wanaokimbia, hawana nidhamu ya kubaki kwenye maeneo yao. Arsenal inaweza kutumia hilo kuwaadhibu wapinzani wao hao.
Gyokeres au Mikel Merino wanaweza kuwavuta Romero na Van de Ven kutoka kwenye eneo hilo la kati, kuwapeleka pembeni na kutoa nafasi kwa viungo Eze au Rice kuingia kwenye eneo hilo la kati kushambulia. Arsenal ndiyo timu hiyo iliyoingia kwenye boksi mara nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ikifanya hivyo mara 388.
Arsenal inaongoza kwenye orodha ya timu zilizoingia mara nyingi ndani ya boksi la wapinzani kwa sababu ya staili yao ya uchezaji, ambapo Namba 9 wao anafanya kazi ya kuwahamisha mabeki wa kati wa timu pinzani kumfuata pembeni na kuacha wazi eneo hilo, kuwaruhusu viungo kuingia kufanya mashambulizi. Romero na Van de Ven watakuwa na kazi kubwa kukwepa mtego.
SPURS ITAFANYAJE
Kocha wa Spurs, Thomas Frank anaweza kukabiliana na uhodari huo wa Arsenal kwa kuwatumia viungo wake wawili wa kati, Joao Palhinha na Rodrigo Bentacur, kushuka chini kuwasaidia mabeki wa kati.
Romero na Van de Ven wanaweza kuondoka kwenda kumbana Namba 9, huku viungo wake wake wa kati wakijaribu kuziba mapengo kwenye upande wa kushoto na kulia kwenye eneo hilo la mabeki wa kati.
Hilo litawafanya Spurs kuwa na wachezaji sita kwenye safu ya ulinzi, huku Frank akilenga kuishambulia Arsenal kwa mashambulizi ya kushtukiza.
Kumdhibiti Bukayo Saka na Leandro Trossard utakuwa msingi mkubwa wa Spurs, kuhakikisha wanawazibia njia za kupita kwa sababu wachezaji hao ni hatari kwenye kutumia nafasi zinazopatikana hata kama ni kwa ufinyu.
MECHI YENYEWE
Martin Odegaard anatazamiwa kurudi uwanjani kwenye kipute hicho, wakati Randal Kolo Muani anaweza kuonekana uwanjani akiwa na amevaa maski. Kocha Arteta atafurahia kurejea kwa nahodha wake huyo kuongeza ufundi kwenye eneo la kushambulia, lakini Spurs ikiamini Muani, ambaye alionekana mazoezini akiwa na maski, anaweza kufanya kitu tofauti uwanjani.
Kwenye rekodi, mechi za Arsenal na Spurs kwenye Ligi Kuu England ni 66 zilizofanyika hadi sasa, ambapo mara 24 zilimalizika kwa timu hizo kutoa sare, huku Arsenal ikionyesha ubabe kwa kushinda mara 27 dhidi ya 15 ilizoshinda Spurs.
Katika ushindi huo wa Arsenal, mara 19 ilifanya kwenye mechi ilizocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani na nane tu ugenini, wakati Spurs yenyewe imeshinda mara 13 nyumbani na mbili tu ilipokwenda kuifuata Arsenal kwao.
Hivyo, kwa rekodi hiyo, Arsenal ina nafasi kubwa ya kuichapa Spurs inapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Emirates. Je, Spurs inapindua kibao? Ngoja tuone.