Arsenal ni vyuma tu
Muktasari:
- Miamba hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta imekuwa bize kwelikweli kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, ambapo hadi sasa imeshawanasa Martin Zubimendi, Noni Madueke, Christian Norgaard na Kepa Arrizabalaga.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL bado inapambana kuboresha fowadi yake, ambapo kinachoelezwa ni kwamba kuna wachezaji watatu inawafukuzia kunasa saini zao kabla ya dirisha kufungwa.
Miamba hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta imekuwa bize kwelikweli kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, ambapo hadi sasa imeshawanasa Martin Zubimendi, Noni Madueke, Christian Norgaard na Kepa Arrizabalaga.
Na ipo kwenye hatua za mwisho kuwasajili beki wa Valencia, Cristhian Mosquera na straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres - ambapo dili zao zitakamilika muda wowote.
Na kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba Arsenal inapiga hesabu za kuwanasa mastaa watatu matata wa kuja kuongeza nguvu kwenye fowadi yao, ikimsaka winga wa Real Madrid, Rodrygo, staa wa Newcastle United, Anthony Gordon na yule wa Crystal Palace, Eberechi Eze. Na kinachoelezwa ni kwamba dili lolote linalohusu mmoja wa mastaa hao watatu likitokea, basi litawahusisha pia Gabriel Martinelli na Leandro Trossard.
Rodrygo amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Arsenal katika dirisha hili baada ya kupoteza namba Real Madrid. Alianzishwa mara moja tu chini ya kocha Xabi Alonso kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu na aliishia tu kukaa benchini kwenye mechi ya kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain katika nusu fainali.
Eze, kwa upande wake ana kipengele kinachotaja Pauni 68 milioni kama pesa inayofaa kuvunja mkataba wake huko Palace na yupo tayari kubadili timu kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, ambapo dhamira yake ni kutaka kuwa mchezaji wa kiwango bora.
MECHI TANO ZA KWANZA ZA ARSENAL EPL 2025-26
-Agosti 17 vs Man United (ugenini)
-Agosti 23 vs Leeds (nyumbani)
-Agosti 30 vs Liverpool (ugenini)
-Septemba 13 vs Nottm Forest (nyumbani)
-Septemba 20 vs Man City (nyumbani)