Arsenal kupigwa za uso kwa Kimmich

Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 30 atakuwa mchezaji huru kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, hivyo alikuwa huru kuzungumza na klabu za ng’ambo zinazomtaka tangu kwenye kipindi cha dirisha la Januari.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ipo kwenye hatari ya kuangukia pua kwenye mpango wa kumsajili kiungo wa Bayern Munich, Joshua Kimmich kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya Mjerumani huyo kufikiria kusaini dili jipya Allianz Arena.
Staa huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 30 atakuwa mchezaji huru kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, hivyo alikuwa huru kuzungumza na klabu za ng’ambo zinazomtaka tangu kwenye kipindi cha dirisha la Januari.
Arsenal ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikizungumza na Kimmich ambaye ameshinda Bundesliga mara nane na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja tangu alipojiunga na Bayern Munich akitokea RB Leipzig 2015.
Lakini, kilichoibuka hivi karibuni ni kwamba Kimmich na mkurugenzi wa michezo wa Bayern, Max Eberl, wamefikia makubaliano juu ya dili jipya.
Na jambo hilo litahitaji kuthibitisha na bodi ya washauri ya klabu hiyo, ambayo ilikutana Alhamisi.
Na kilichofikiwa kwenye kikao hicho ni kwamba mabosi wa Bayern wamesitisha suala hilo na sasa ni kiungo mwenyewe muda wowote anaweza kusaini dili jipya.
Sambamba na kuhitajika na Arsenal, huku akiwa na makubaliano ya mdomo na Bayern, Kimmich ana ofa nyingine mezani kutoka kwa Paris Saint-Germain. Miamba hiyo ya Ufaransa, PSG imempa ofa ya kumpa mkataba Kimmich hadi 2029.