Guardiola awatishia nyau Arsenal
Muktasari:
- Man City ilikuwa ikikabiliwa na pengo la pointi tisa kwenye mbio za ubingwa wakati Dominik Szoboszlai alipofunga bao la kuvutia kwa mpira wa adhabu. Lakini, Bernardo Silva alisawazisha dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho na penalti ya dakika za majeruhi ya Erling Haaland ilitosha kuipa Man City ushindi na pointi tatu muhimu.
MANCHESTER, ENGLAND:PEP Guardiola ameapa kuwa Manchester City itaendelea ‘kupumua shingoni mwa Arsenal’ baada ya ushindi wao wa kushangaza wa dakika za mwishoni dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield, Jumapili.
Man City ilikuwa ikikabiliwa na pengo la pointi tisa kwenye mbio za ubingwa wakati Dominik Szoboszlai alipofunga bao la kuvutia kwa mpira wa adhabu. Lakini, Bernardo Silva alisawazisha dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho na penalti ya dakika za majeruhi ya Erling Haaland ilitosha kuipa Man City ushindi na pointi tatu muhimu.
Kisha, katika mwisho wa vurugu, Gianluigi Donnarumma aliokoa kwa ustadi mkubwa jaribio la nyota wa Liverpool, Alexis Mac Allister, kabla ya Man City kushuhudia bao lao la tatu la kuchekesha likikataliwa.
Man City sasa iko nyuma ya Arsenal kwa pointi sita na inaweza kupunguza tofauti hiyo endapo itawachapa Fulham, Jumatano.
Kocha Guardiola alisema: “Kitu pekee tunachoweza kufanya sasa ni kupumua shingoni mwa Arsenal na kuwepo hapo. Wakilala, wakifanya makosa, basi tunapaswa kuyatumia. Ni pengo kubwa, lakini mambo mengi bado yanaweza kutokea. Zimesalia mechi 13 za Ligi Kuu kutokana na uzoefu wangu mdogo, huo ni muda mrefu sana.”
Nahodha Bernardo, aliyekuwa kichocheo cha kurejea kwao, alisema Man City walilazimika kushinda ili kudumisha matumaini yao ya ubingwa, aliposema: “Kikosi kizima kilijua kabla ya mechi kuwa tukipoteza, huenda mbio za ubingwa zingekuwa zimekwisha. Arsenal bado iko kwenye nafasi nzuri zaidi kuliko sisi, lakini tulihisi lazima tushinde mechi hii. Hii sasa inatuweka karibu kidogo, matumaini bado yapo.”
Guardiola, akiwa amepumua kwa afueni, aliongeza: “Tumeshinda, hatimaye tumeshinda Anfield.”
“Tunahitaji ushindi kama huu kwa sababu bado tuna mambo mengi ya kupigania, ubingwa wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Carabao.”