Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal kuingia sokoni Januari 2026

ARTETA Pict

Muktasari:

  • Iko hivi, kocha Mikel Arteta atafungua milango ya kupokea ofa ya kuwapiga bei mastaa wa nne wa kikosi hicho cha Arsenal, kwamba kama kutakuwa na timu nyingine inayohitaji saini ya mchezaji yeyote kwenye orodha tajwa, anakaribishwa mezani.

LONDON, ENGLAND: USHAWAHI kupita kwenye gulio? Kuna lugha zao kule kwenye uuzwaji wa bidhaa ikiwamo ya sagula sagula, kwamba mnunuzi chagua unachokitaka. Hicho ndicho inachokwenda kufanya Arsenal kwenye dirisha lijalo la Januari.

Iko hivi, kocha Mikel Arteta atafungua milango ya kupokea ofa ya kuwapiga bei mastaa wa nne wa kikosi hicho cha Arsenal, kwamba kama kutakuwa na timu nyingine inayohitaji saini ya mchezaji yeyote kwenye orodha tajwa, anakaribishwa mezani.

Kwenye orodha ya mastaa ambao Arsenal imewaweka sokoni kwenye dirisha la Januari, yupo pia kinda anayeibukia kwa kasi sana kwenye kucheza soka la kiwango bora kabisa uwanjani, Ethan Nwaneri.

Kinachoripotiwa ni kwamba, kwa timu nyingine yoyote inayohitaji saini ya Nwaneri inaweza kupeleka maombi yao hata kama ni ya mkopo, yanakubalika na miamba hiyo ya Emirates ilimradi biashara ifanyike kwenye dirisha la Januari.

Nwaneri, 18, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Arsenal chini ya kocha Arteta, alipoanza kukitumikia timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 15. Hata hivyo, ndani ya msimu huu bado hajaanzishwa kwenye mechi yoyote na katika kuendeleza kipaji chake, Arteta anafikiria kumtoa hata kwa mkopo kwenye dirisha la Januari.

ART 01

Ukimweka kando Nwaneri, mchezaji mwingine wa Arsenal atakayekuwa sokoni kwenye dirisha la Januari ni beki kiraka, Ben White, huku winga mwenye kasi ya ajabu kutoka Brazil, Gabriel Martinelli, naye milango ya kupokea ofa kumhusu ikiwekwa wazi na kuna uwezekano akatimkia zake huko Saudi Arabia.

Martinelli amepoteza namba kwenye kikosi kinachoanza cha Arsenal msimu huu baada ya ujio wa winga Noni Madueke kutokea Chelsea kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Mshambuliaji Gabriel Jesus, ambaye pia ni Mbrazili, naye yupo kwenye orodha hiyo ya wanaofunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha la Januari endapo kama ofa italetwa kumhusu. Arsenal inataka kuachana na Jesus kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Fowadi huyo kwa sasa anakaribia kupona maumivu ya goti (ACL) aliyopata msimu uliopita kwenye mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA.

ART 02

Jesus alifunga mabao manne katika mechi mbili alizokabiliana na Crystal Palace kwenye Kombe la Ligi na Ligi Kuu England kabla ya kupata pigo hilo la kuumia lililomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Arsenal matumaini yao ni kwamba Jesus atakuwa fiti kwa kiwango cha kutosha kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya baridi ambalo litafunguliwa Januari Mosi.

Na kama ofa nzuri italetwa, basi Arsenal haitasita kumfungulia mlango wa kutokea straika huyo ambaye alitua Emirates mwaka 2022 na kama atashindwa kuondoka Januari, basi mwisho wa msimu ni lazima.

Arsenal ilitumia Pauni 250 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kunasa huduma za mastaa Kepa Arrizabalaga, Martin Zubimendi, Christian Norgaard, Noni Madueke, Cristhian Mosquera, Viktor Gyokeres na Eberechi Eze.

Na sasa inataka kupunguza kikosi chake kwa kuondoa wachezaji ambao hawapewi nafasi ya kucheza. Arsenal itarejea uwanjani kwenye mechi ya Ligi Kuu England, Jumapili itakapokuwa nyumbani uwanjani Emirates kukabiliana na mahasimu wao Tottenham Hotspur kwenye kipute cha North London Derby.