Eze adai kazi ya mkewe inamtuliza
Muktasari:
- Eze, aliyehamia Emirates majira ya joto yaliyopita kutoka Crystal Palace kwa dau la awali la Pauni 60 milioni, kwa sasa anajaribu kuipambania Arsenal kwenda kutwaa mataji manne msimu huu.
LONDON, ENGLAND: STAA wa Arsenal, Eberechi Eze, amesema kazi ya mkewe kama muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) imempa “ukumbusho wa uhalisia” kuhusu presha ya kufuatilia na kushinda mataji.
Eze, aliyehamia Emirates majira ya joto yaliyopita kutoka Crystal Palace kwa dau la awali la Pauni 60 milioni, kwa sasa anajaribu kuipambania Arsenal kwenda kutwaa mataji manne msimu huu.
Shinikizo liko juu ya The Gunners kufanya vizuri kwani mara ya mwisho kuinua taji chini ya Mikel Arteta ilikuwa mwaka 2020.
Na Eze ameeleza jinsi mkewe, mrembo Naima Corbin, humsaidia kubaki mnyenyekevu kutokana na presha kubwa anayokumbana nayo kazini kwake.
Kiungo huyo mshambuliaji alisema: “Narudi nyumbani nikiwa nawaza kuhusu mambo kadhaa. Halafu napata ukumbusho wa uhalisia kutoka kwa mke wangu, anafanya kazi ICU. Kwa kweli, napenda sana sehemu hiyo ya maisha yangu. Inakushusha chini na kukufanya uwe mnyenyekevu. Bado nitatazama sana mpira nyumbani kwa sababu naupenda sana, lakini pia kuna nyakati unahitaji kujitenga kabisa nao, jambo ambalo ni zuri. Bila hata kugundua, unaweza kupunguza uzito wa mambo kidogo na kupunguza hisia kali kuhusu kila kitu.”
Eze amekuwa na mwanzo wa mchanganyiko tangu ajiunge na Arsenal akitokea upande mwingine wa London. Nyota huyo wa England alifunga hat-trick katika dabi ya Kaskazini mwa London mwezi Novemba, lakini hivi karibuni amekuwa akipata dakika chache za kucheza.
Kiungo huyo amekiri kwamba imechukua muda kuzoea mfumo mpya wa mchezo chini ya Arteta.
Eze alisema: “Kuna umakini mkubwa sana kwenye maelezo kuhusu jinsi tunavyoikaribia mechi na kujiandaa kwa ajili ya mechi, na ni zaidi ya nilivyozoea. Hivyo ilihitaji muda kuzoea, lakini unaona jinsi unavyopaswa kuwa tayari ili kucheza katika kiwango hiki. Ni jambo la lazima, lakini labda lilihitaji muda kidogo kuzoea.”