Arsenal itakavyokwenda kuboreshwa iwe ya kinyama zaidi msimu ujao

Muktasari:

  • Arsenal imekuwa na mwendelezo mzuri sana ndani ya uwanja kwa miaka ya karibuni, ikiwa makini kwenye usajili wa wachezaji wapya na linalosemwa ni kwamba wamepanga kuleta wakali wengine watakaokuja kufanya tofauti kubwa katika kikosi hicho cha Emirates.

LONDON, ENGLAND: Arsenal imeelekeza akili kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England ikijaribu kupimana ubavu na Manchester City hadi filimbi ya mwisho msimu huu. Hata hivyo, huko nyuma ya pazia kuna mambo yanafanyika juu ya ishu ya usajili wa kujua ni mchezaji gani wa kuletwa kwenye kikosi wakati wa dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Arsenal imekuwa na mwendelezo mzuri sana ndani ya uwanja kwa miaka ya karibuni, ikiwa makini kwenye usajili wa wachezaji wapya na linalosemwa ni kwamba wamepanga kuleta wakali wengine watakaokuja kufanya tofauti kubwa katika kikosi hicho cha Emirates.

Arsenal haina kikosi kipana kulinganisha na Man City, lakini itahitaji kuboresha kikosi chake kwa ajili ya kucheza kwa mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi litafunguliwa Juni 14 na litafungwa Septemba 2, kitu ambacho kitawapa mkurugenzi wa michezo, Edu na kocha Mikel Arteta muda wa kutosha wa kuamua aina ya wachezaji inaowahitaji kuwanasa kwenye kikosi chao.

Katika kuifanya Arsenal kuwa ya kibabe msimu ujao, hiki ndicho ambacho miamba hiyo ya Emirates inapaswa kufanya ili kuwa na kiwango matata na kushindana kwenye msimu ujao 2024/25.


WAPIGWE KIBUTI

Arteta amekuwa na kikosi chake cha wachezaji wachache, ambao amehakikisha wanakuwa kwenye ubora mkubwa wa kumpa matokeo mazuri ndani ya uwanja kwa msimu huu. Viwango vya juu kwenye mechi mfululizo, huku ikiwa na bahati ya kutosumbuliwa na majeruhi yoyote, jambo hilo limeifanya Arsenal kuwa na nguvu kubwa kwenye ligi, lakini kuna ulazima mkubwa wa kupunguza wachezaji kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Mohamed Elneny na Cedric Soares wametumika mara chache sana msimu huu, wakicheza mechi sita tu kwenye michuano yote. Na Elneny amekuwa kwenye kikosi cha Arsenal tangu mwaka 2016, sasa akiwa na umri wa miaka 31 ni wakati wakupewa mkono wa kwaheri, huku mkataba wake ukifika ukomo Juni.

Cedric naye anaelekea mwisho wa mkataba wake, hivyo wawili hao wote wanaweza kuondoka bure. Kisha kwenye ile orodha ya wachezaji waliotolewa kwa mkopo. Kieran Tierney kuna nyakati alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Arsenal, lakini mahitaji ya kocha Arteta kwa mabeki wake wa pembani yamemfanya Mskochi huyo kupoteza nafasi mbele ya Oleksandr Zinchenko, Takehiro Tomiyasu na Jakub Kiwior. Hivyo, Arsenal inaweza kuchukua uamuzi wa kumuuza Tierney. Amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake huko Arsenal, lakini huko alipo Real Sociedad, anakocheza kwa mkopo, amekuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza, hivyo anaweza kuondoka tu mwishoni mwa msimu. Nuno Tavares hajafika kwenye viwango vinavyotakiwa na Arsenal. Albert Sambi Lokonga anapata nafasi ya kucheza huko Luton, hivyo Arsenal hana nafasi baada ya kiungo hiyo ya miamba hiyo ya Emirates kuwa na wakali Declan Rice, Thomas Partey na Jorginho. Marquinhos ni kijana, lakini anaweza kuuzwa. Aaron Ramsdale naye anaweza kufunguliwa mlango wa kutokea, akapeta nafasi ya kucheza kwingineko baada ya kushindwa kumshawishi kocha Arteta ampange mbele ya David Raya. Arsenal pia itamuuza Gabriel Jesus.


WABAKIZWE

Kipa Raya anacheza Arsenal kwa mkopo akitokea Brentford, lakini kwa kiwango chake cha msimu huu bila ya shaka miamba hiyo ya Emirates itashawishika kumbakiza. Wana kipengele kinachowalazimisha kumsajili jumla kwa Pauni 27 milioni, kitu ambacho kwa uwezo wake wa uwanjani, ni kiasi kidogo cha pesa.

Jorginho alisaini mkataba wa miezi 18 wa kuendelea kubaki kwenye klabu hiyo, ambapo Arsenal inahitaji kuendelea kubaki na huduma yake kutokana na uzoefu wake. Uhakika ni mkubwa atapata ofa ya dili jipya, huku Thomas Partey, ambaye mkataba wake utakaokwisha Juni 2025, Arsenal inaweza kushawishika kumbakiza ili aendelee kucheza vyema na Declan Rice.


Waletwe fasta

Raya ni kipa namba moja, lakini kama Arsenal itampiga bei Ramsdale, basi itahitaji kipa mwingine wa akiba. Karl Hein mkataba wake unakwisha mwisho wa msimu na Arthur Okonkwo kwa sasa yupo kwa mkopo Wrexham. Kwa makipa hao wawili, hakuna mwenye uwezo wa kuwa namba mbili, hivyo miamba hiyo ya Emirates, imekuwa ikihusishwa na Patrick Schulte wa Columbus Crew ya Marekani. Kipa huyo anasakwa na timu nyingi ikiwamo Man United.

Kwenye safu ya ushambuliaji kwa sababu itaachana na Jesus, Arsenal inahitaji kufanya maboresho kwenye eneo hilo na kwenye rada yao inatajwa kuwapo na majina ya straika wa Newcastle United, Alexander Isak na wa Brentford, Ivan Toney. Inamsaka pia Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon na straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko. Arsenal pia itahitaji kuongeza beki mwingine kwenye dirisha lijalo. Msimu huu imekuwa kwenye ulinzi bora mbele ya mabeki Gabriel Magalhaes, William Saliba na Ben White, ambaye kwa siku za karibuni amekuwa akitumika kwenye upande wa kulia.

Beki mwingine kiraka anahitajika kwenye kikosi hicho hasa baada ya Jurrien Timber kuwa na majeruhi ya muda mrefu. Kwenye hilo, kinachoelezwa ni kwamba wanahitaji saini ya Marc Guehi wa Crystal Palace na yule beki wa Sporting, Ousmane Diomande.