Arsenal bana, hadi mashabiki visu si kitoto

LONDON, ENGLAND. MREMBO Kim Kardashian aliwaacha mashabiki wa Arsenal wakimeza mafunda ya kutosha tu ya mate wakati walipomshuhudia akiwa jukwaani uwanjani Emirates wakati vinara hao wa Ligi Kuu England walipokuwa kwenye majukumu ya Europa League kwa kucheza dhidi ya Sporting Lisbon.

Lakini, mrembo huyo aliyekuwa mke wa zamani wa rapa mtata, Kanye West hakuwa na bahati, kwani uwepo wake jukwaani haukusaidia Arsenal kushinda na badala yake ilichapwa kwa penalti 5-3 na kutupwa nje kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

Na baada ya hapo, baadhi ya mashabiki wa Arsenal waliomba mrembo huyo asirudi tena kutazama mechi zao za Ligi Kuu England, asije akaleta mkosi kama ambao umewatokea kwenye Europa League.

Hata hivyo, ukweli utabaki palepale, mrembo Kim K anaendeleza orodha ya mashabiki warembo na maarufu wanaoshabikia Arsenal.

Hii hapa orodha ya warembo matata kabisa na walio maarufu ambao wamekuwa wakiishabiki timu hiyo inayovaa jezi nyekundu na nyeupe.


IVANA KNOLL

Yule mrembo aliyetamba kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, Ivana Knoll ni shabiki wa Arsenal. Mrembo Ivana, ambaye ni Mcroatia, alitesa sana huko Qatar na baadaye ifahamika anaishabiki Arsenal. Mrembo huyo mwanamitindo, anayeishi Miami, Marekani, alishuhudia mechi ya Arsenal na Manchester City, naye hakuwa na bahati ya ushindi, kwani The Gunners ilichapwa 3-1


KIM KARDASHIAN

Mrembo Kim alikuwapo jukwaani wakati Arsenal ikimenyana na Sporting kwenye Europa League uwanjani Emirates, Alhamisi iliyopita. Kim aliwashtua wengi baada ya mwanaye wa kiume, Saint kuonekana akiwa amevaa jezi ya Arsenal. Kama ilivyo kwa Ivana, hata Kim naye mechi yake aliyokwenda uwanjani kuwashuhudia Arsenal ikicheza, haikuisha vizuri, timu yao iliyolewa kwenye michuano ya Europa League.


DIDO

Mwimbaji huyo Mwingereza, ambaye jina lake halisi ni Florian Cloud de Bounevialle O’Malley Armstrong, amekuwa shabiki wa Arsenal tangu alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Akizungumzia mapenzi yake kwa Arsenal, Dido alisema: “Tangu nikiwa na umri wa miaka mitatu, mwaka 1974, baba yangu alinichukua kwenda kuwatazama Arsenal. Ilikuwa ni kama dini kwake.” Mara kadhaa Dido ameonekana Emirates kuishangilia Arsenal.


CHARLIZE THERON

Mwaka 2009 Charlize alitangaza kwamba anaisapoti Chelsea, lakini miaka miwili baadaye, mwigizaji huyo mrembo kabisa, aliyeshinda Tuzo ya Oscar, alionekana akiwa na jezi ya Arsenal uwanjani Emirates. Na kwa Charlize, mambo yalikuwa matamu kwake, wakati aliposhangilia akiwa uwanjani Arsenal ilipoichapa Manchester United bao 1-0. Mrembo Charlize ni Msauzi.


DEMI MOORE

Kwa mujibu wa OHFact.com, Demi anapenda kutazama mechi za Arsenal na amekuwa akienda uwanjani Emirates mara zote anapokuwa London. Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 60 aliwahi kuolewa na Bruce Willis na baadaye Ashton Kutcher. Mwaka jana, Demi Moore alisema anapenda kutazama vitu vinavyovutia na pengine hilo ndilo linalomfanya kwenda uwanjani kuitazama Arsenal ikicheza.


GWYNETH PALTROW

Mrembo Gwyneth alikuwa kwenye wakati mgumu wa ushabiki wake wa Arsenal mwaka 1999, wakati alipolazimika kuigiza kwenye filamu moja na shabiki wa Chelsea. Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 50 alicheza filamu na Ralph Fiennes, ambaye ni shabiki mkubwa wa Chelsea katika filamu yao iliyokwenda kwa jina la Shakespeare In Love. Inasemekana mrembo huyo alikuwa akiimba nyimbo za Arsenal kumkera tu Fiennes.


GISELE BUNDCHEN

Sawa, unaweza usiwe na uhakika sana, lakini mrembo Gisele alipiga picha akiwa ameshikilia jezi ya Arsenal alipoweka pozi na gwiji wa miamba hiyo ya Emirates, Thierry Henry. Hiyo ilikuwa mwaka 2007, kipindi hicho mrembo Gisele alipokuwa kisura wa Ebel, ambayo ilikuwa mshirika wa klabu ya Arsenal. Katika tukio hilo, mrembo Gisele alionekana mwenye furaha alipokuwa akikabidhiwa jezi ya Arsenal na staa Henry.