Antony agomea ofa ya tatu
Muktasari:
- Man United imekuwa ikifanya majaribio ya kuachana na Antony, 25, tangu dirisha hili la majira ya kiangazi lilipofunguliwa.
WROCLAW, POLAND: WINGA Antony amegomea nafasi nyingine ya kuondoka Manchester United kwa mara ya tatu dirisha hili la majira ya kiangazi akiendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kurudi Real Betis.
Man United imekuwa ikifanya majaribio ya kuachana na Antony, 25, tangu dirisha hili la majira ya kiangazi lilipofunguliwa.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim ameshamwambia staa huyo aliyecheza mechi 16 kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil aondoke kwenye timu yake sambamba na wachezaji wengine wanaotimiza mastaa watano, akiwamo Marcus Rashford, Alejandro Garnacho, Jadon Sancho na Tyrell Malacia. Mastaa hao watano hakuna hata mmoja aliyesafiri na timu kwenye ziara ya mechi za pre-season huko Marekani, ambapo Man United ilifanikiwa kubeba taji la Premier League Summer Series.
Kwenye orodha ya mastaa hao ni Rashford pekee aliyepata timu hadi sasa baada ya kujiunga na Barcelona kwa mkopo wa msimu mmoja. Kuhusu Antony, Man United haitaki kumwondoa kwa muda, ikitaka aondoka moja kwa moja ili kupata Pauni 30 milioni, ambazo ndiyo bei ya wanayomuuza.
Hilo ni anguko la asilimia 65 kutoka kwa Pauni 86 milioni ambazo Man United ililipa huko Ajax kunasa huduma yake miaka mitatu iliyopita. Winga huyo anataka kurudi kujiunga Betis, ambako alicheza kwa mkopo msimu uliopita, lakini klabu hiyo ya Hispania bado haina pesa ya kumudu gharama yake.
Antony hajaishiwa ofa, kuna timu nyingi zinamtaka ikiwamo za Brazil, Botafogo na Sao Paulo. Na kinachoripotiwa staa huyo amekataa ofa ya tatu.
Miamba ya soka ya Saudi Arabia, Al-Nassr, ambako anacheza supastaa wa zamani wa Man United, Cristiano Ronaldo imeleta ofa ya kumsajili Antony, lakini Mbrazili huyo amegomea ofa yao.
Taarifa za kutoka Hispania zinafichua kwamba Antony anachotaka ni kurudi kujiunga na Betis na hataki kujiunga na timu nyingine. Na sasa staa huyo yupo tayari kushusha mshahara wake hadi Pauni 4 milioni kwa mwaka ili kwenda kujiunga na miamba hiyo ya La Liga inayonolewa na Manuel Pellegrini.