Ange Postecoglou anatajwa tajwa huko Celtic
Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na Nottingham Forest anapewa nafasi kubwa ya kurudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani huko Scotland baada ya Rodgers kuchukua uamuzi wa kujiuzulu katika kikosi hicho cha Parkhead.
GLASGOW, SCOTLAND: ANGE Postecoglou ametajwa kuwamo kwenye orodha ya makocha wanaopewa kipaumbele kwenda kuinoa Celtic baada ya Brendan Rodgers kuachia ngazi.
Kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na Nottingham Forest anapewa nafasi kubwa ya kurudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani huko Scotland baada ya Rodgers kuchukua uamuzi wa kujiuzulu katika kikosi hicho cha Parkhead.
Rodgers, 52, ameamua kuachana na Celtic kwa mara ya pili baada ya mambo yake kuwa magumu msimu huu na Hearts inaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nane.
Martin O’Neill na Shaun Maloney wataiongoza Celtic kama makocha wa muda, wakati mabosi wa klabu hiyo wakifanya mchakato wa kuleta kocha mkuu mpya.
Na hilo halikuchua muda kuanza kumhusisha Postecoglou, ambaye wacheza kamari wanaamini kocha huyo anaweza kurudi kuinoa timu hiyo baada ya mambo kwenda kombe Ligi Kuu England.
Makocha wengine wanaohusishwa na wacheza kamari ni Robbie Keane, Ole Gunnar Solkskjaer, Kjetil Knutsen, Craig Bellamy, Damien Duff na Erik Ten Hag.
Postecoglou kwa sasa hana kazi baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea huko Nottingham Forest, alikofanya kazi kwa siku 39.
Hiyo ilikuwa mara ya pili ndani ya miezi minne kocha huyo kuonyeshwa mlango wa kutokea, maana alifutwa kazi pia Spurs, Juni mwaka huu. Postecoglou alifanya makubwa Celtic kwa miaka miwili aliyokuwa kwenye timu hiyo na kuwa kipenzi cha mashabiki baada ya kubeba mataji matano katika misimu hiyo, ikiwamo mataji matatu katika msimu wake wa pili.