Andoni Iraola aihidi makubwa Liverpool
Muktasari:
- Iraola mwenye umri wa miaka 44 alisaini mkataba wa miaka miwili mwezi uliopita baada ya kuwa na mafanikio makubwa ndani ya Bournemouth, alikoitumikia kwa misimu mitatu.
KOCHA mpya wa Liverpool, Andoni Iraola, amesema lengo lake kubwa ni kuijenga timu ambayo mashabiki watajivunia, huku akisisitiza yupo tayari kukabiliana na shinikizo la kuinoa moja ya klabu kubwa zaidi duniani.
Iraola mwenye umri wa miaka 44 alisaini mkataba wa miaka miwili mwezi uliopita baada ya kuwa na mafanikio makubwa ndani ya Bournemouth, alikoitumikia kwa misimu mitatu.
Liverpool ilimaliza nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, nafasi moja mbele ya Bournemouth, kabla ya klabu hiyo kumfuta kazi Arne Slot mwishoni mwa Mei.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari tangu ateuliwe, Iraola amesema jambo la kwanza analotaka kulirejesha ni uhusiano wa karibu kati ya timu na mashabiki wa Anfield.
"Liverpool ni klabu inayojengwa kupitia muunganiko kati ya timu na mashabiki. Lazima tuwe karibu nao na tuwape sababu ya kujivunia timu yao," amesema.
Kocha huyo wa Hispania alisema tayari amewahi kushuhudia nguvu ya mashabiki wa Anfield akiwa kocha wa Bournemouth, hasa katika mchezo ambao Federico Chiesa aliifungia Liverpool bao la ushindi mwanzoni mwa msimu uliopita.
"Unaweza kuhisi nguvu za uwanja ule. Ningependa tuzipate hisia hizo kila mechi tunayocheza nyumbani, lakini hilo litaanza na sisi wenyewe uwanjani."
Ameongeza kuwa Liverpool yake itakuwa timu inayocheza kwa nguvu, kasi na kushambulia moja kwa moja ili kuwafanya mashabiki wajitambulishe nayo.
"Tunataka kuwa timu inayopambana, yenye presha kubwa, inayocheza kwa kasi na kushambulia moja kwa moja. Hivyo mashabiki watafurahia kutuunga mkono."
"Nipo tayari kwa changamoto ya Liverpool"
Iraola, ambaye kabla ya Bournemouth aliwahi kuzinoa AEK Larnaca, Mirandés na Rayo Vallecano, amesema anaelewa ukubwa wa jukumu alilopewa.
"Nipo tayari. Najua Liverpool ni klabu kubwa sana. Kila neno na kila uamuzi wangu vitachunguzwa kwa makini, lakini sitaki kuishi kwa hofu ya kukosea."
Aliongeza kuwa hataki kujitenga na maisha ya jiji la Liverpool licha ya majukumu yake.
"Sitaki kuishi kati ya uwanja wa mazoezi na nyumbani pekee. Nataka kutembea mjini, kulifahamu jiji na kufurahia sehemu zake mbalimbali. Hiyo ni sehemu ya uzuri wa kuwa kocha wa Liverpool."
Mkataba wa miaka miwili si tatizo
Iraola pia alizungumzia mkataba wake wa miaka miwili, ambao ni mfupi ukilinganisha na mikataba mingi ya makocha wa vilabu vikubwa.
Kocha huyo alisema kwake muda wa mkataba si jambo muhimu, kwani anaamini kocha anatakiwa kuthibitisha uwezo wake kila msimu.
"Kwa upande wangu, mikataba ya makocha haina maana kubwa. Sitaki kubaki sehemu kwa sababu tu nina mkataba."
"Nimesaini miaka miwili, lakini kazi ya ukocha ni ya msimu mmoja mmoja. Natumaini nitadumu hapa zaidi ya miaka miwili, kwa sababu hiyo itamaanisha nimeifanya kazi yangu vizuri."
Iraola alisisitiza kuwa katika klabu kubwa kama Liverpool, kila kocha anapaswa kujipatia haki ya kuendelea kila mwaka kupitia matokeo na kiwango cha timu, jambo ambalo amesema ndilo falsafa aliyofuata katika maisha yake yote ya ukocha.