Ancelotti achimba mkwara Brazil
Muktasari:
- Ancelotti, ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Selecao, Mei mwaka huu baada ya kutua hapo akitokea Real Madrid ana majukumu mazito mezani yake kwa ajili ya kuipa taji la dunia timu hiyo.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: KOCHA, Carlo Ancelotti ameahidi kwamba Brazil itawasha moto kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kufuzu michuano hiyo kwa rekodi mbaya.
Ancelotti, ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Selecao, Mei mwaka huu baada ya kutua hapo akitokea Real Madrid ana majukumu mazito mezani yake kwa ajili ya kuipa taji la dunia timu hiyo.
Mtaliano huyo akiwapata uzoefu wa mara ya kwanza kwenye soka la kimataifa, alishuhudia chama lake la Brazil likikutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Bolivia.
Kichapo hicho kimeifanya Brazil kumaliza nafasi ya tatu kwenye fungu la timu za Amerika Kusini, nyuma ya Argentina, Ecuador, Colombia na Uruguay. Brazil imefuzu fainali hizo za mwakani zitakazofanyika Canada, Marekani na Mexico, lakini Ancelotti ameandikisha rekodi mbaya ya miamba hiyo kwenye kufuzu fainali za dunia.
Brazil kumaliza nafasi ya tano kwenye mchakato wa kufuzu Amerika Kusini unaojumuisha timu 10 ni ya chini zaidi tangu ulipoanzishwa CONMEBOL mwaka 1998 baada ya kuvuna pointi 28.
Hata hivyo, imemaliza pointi sawa na Colombia na Uruguay, ambazo zimekuwa juu yao kutokana na kuwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufunga na pointi moja nyuma ya timu iliyoshika nafasi ya pili, Ecuador.
Awamu yao nyingine waliomaliza chini ilikuwa kwenye kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2002, ilipomaliza nafasi ya tatu, lakini ilikwenda kubeba ubingwa huo huko Japan na Korea Kusini, ambapo lilikuwa taji lao la tano ya dunia, wakiamini wanaweza kurudia makali hayo mwakani.
“Hii mechi ilikuwa ngumu sana, kimbinu na kifiziki,” alisema Ancelotti baada ya mechi hiyo iliyopigwa Bolivia kwenye Uwanja wa Municipal de El Alto, ulopita futi 13,000 kutika usawa wa bahari, ambako kumekuwa na hali ya hewa korofi kwa wachezaji.
“Hii ilikuwa mechi maalumu. Tutajiandaa na mechi zijazo na tutakwenda Kombe la Dunia tukiwa kwenye ubora mzuri.”