Amorim: Msikonde, tutarudi kivingine

Muktasari:
- Hata hivyo, baadhi ya mastaa wa timu hiyo hawakuonekana kuwa na furaha kabisa wakati kocha wao alipokuwa akiwachana mmoja baada ya mwingine mbele ya maelfu ya mashabiki uwanjani Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya kumaliza msimu vibaya, timu ikiweka rekodi za hovyo kabisa kwenye Ligi Kuu England.
Hata hivyo, baadhi ya mastaa wa timu hiyo hawakuonekana kuwa na furaha kabisa wakati kocha wao alipokuwa akiwachana mmoja baada ya mwingine mbele ya maelfu ya mashabiki uwanjani Old Trafford.
Man United ilihitimisha msimu wake mbaya kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa. Na huo ulikuwa ushindi wao wa 11 kwa msimu huu - ambao ulitanguliwa na maandamano ya mashabiki nje ya Uwanja wa Old Trafford wakipinga mambo ya wamiliki. Amad Diallo na Christian Eriksen ndiyo waliofunga mabao.
Baada ya mechi hiyo, Amorim alichukua kipaza sauti na kuzungumza na mashabiki uwanjani.
Kocha huyo alisema: “Kwanza kabisa, nataka kuwaomba radhi. Hii timu imewahuzunisha sana. Pili, nataka kuwashukuru. Tunashukuru kwa sapoti yenu msimu huu.”
Kocha huyo aliongeza: “Nafahamu ilikuwa ngumu sana kutusapoti kwenye mechi nyingi. Lakini, sasa yatupaswa kufanya uamuzi au tubaki tu tukifikiria mambo yaliyopita. Huu msimu umeshapita, umekwisha.
Tulumbane au tushikamane kwa pamoja na kusonga mbele.”
Amorim alitoa kauli hiyo mbele ya mashabiki 74,000 aliposema: “Miezi sita iliyopita, kwenye mechi zangu tatu za kwanza, tulishinda mbili na sare moja, niliwaambia kuna janga linakuja. Hii leo, baada ya msimu huu wa majanga, ninachotaka kuwaambia nyakati njema zinakuja.”
Kauli hiyo iliibua shangwe kubwa kwa mashabiki, kabla ya Amorim kumalizia kwa kusema: “Kama kuna klabu moja duniani ambayo ilithibitisha hili huko nyuma na kuvuka vikwazo vyote, majanga yote basi ni klabu yetu hii Manchester United Football Club.
“Nataka kuwaomba radhi wachezaji wangu pia. Wakati mwingine sikuwa sahihi, lakini siku zote nilitaka kuwa wazi kwenu. Asanteni sana, tutaonana msimu ujao.”
Hotuba hiyo ilipokewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa uwanjani hapo. Lakini, kwa upande wa wachezaji, wakati baadhi wakipiga makofi, wengine walibaki kimya na kuweka mikono nyuma.
Amorim alijiunga na Man United kuchukua mikoba ya Erik ten Hag, Novemba mwaka jana, ambapo timu hiyo ilifanya vibaya, ikimaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikivuna pointi 42 tu.