Amorim: Man u tusajili? No
Muktasari:
- KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amefuta mpango wa kuingia sokoni kusajili wachezaji ambao wapo huru ili kuokoa jahazi baada ya kikosi hicho kuandamwa na majeruhi wengi.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amefuta mpango wa kuingia sokoni kusajili wachezaji ambao wapo huru ili kuokoa jahazi baada ya kikosi hicho kuandamwa na majeruhi wengi.
Mabingwa hao mara 20 wa England walikosa wachezaji 12 wa kikosi cha kwanza katika mechi dhidi ya Tottenham Hotspur wikiendi iliyopita kutokana na kuwa majeruhi na wengine kuwa wagonjwa na kwenye mechi ya jana Jumamosi, ilitarajia kukosa wachezaji tisa wakati ilipokwenda kumenyana na Everton uwanjani Goodison Park katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Lisandro Martinez na Amad Diallo hawataonekana tena uwanjani hadi mwisho wa msimu, huku kukiwa na hofu huenda Mason Mount asicheze tena hadi mwisho wa msimu.
Kobbie Mainoo atakosekana uwanjani na kwamba Mwingereza huyo atarudi Aprili na nje ya Victor Lindelof kwenye benchi la Man United katika mechi ya Spurs kulikuwa na wachezaji kibao kutokea kwenye akademia ya klabu hiyo. Hata hivyo, Amorim alisema tena kwa msisitizo kwamba Man United haina mpango wa kusajili wachezaji huru ili kuongeza nguvu kwenye kikosi, aliposema: “Hapana. Hakuna huo mpango. Tuna vijana wengi, tutafanya kazi na vijana. Tumewekeza nguvu kwenye hilo kama klabu hasa tunapokuwa na majeruhi wengi.
“Tutawatumia wachezaji vijana. Kama si majeruhi, hatutakuwa na nafasi ya kuwapa waonyeshe ubora wao. Nadhani tunapaswa kuwekeza zaidi kwenye hatima ya timu hii kwa vijana kwa sababu historia ya klabu hii inabainisha hilo.”
Kwenye mchezo wa leo Man United ilipata mzuka baada ya Leny Yoro, Christian Eriksen na Manuel Ugarte kurudi kwenye kikosi cha kwanza, lakini bado kulikuwa na nafasi ya wachezaji wa akademia kupewa nafasi.
Miongoni mwa makinda hao walitarajia kupewa nafasi ni Chido Obi, 17, ambaye alichezeshwa kwa dakika tatu za majeruhi katika mechi ya Spurs.