Amorim asema kitu kuhusu Mainoo
Muktasari:
- Mainoo aliishia tu kubaki benchini bila ya kutumika kwa mara ya nne msimu huu baada ya kukosa pia mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United iliyofanyika usiku wa Alhamisi iliyopita.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amekubali kwamba kitendo cha Kobbie Mainoo kukosa muda wa kutosha wa kucheza umemfanya mchezaji huyo aathirike kisaikolojia.
Mainoo aliishia tu kubaki benchini bila ya kutumika kwa mara ya nne msimu huu baada ya kukosa pia mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United iliyofanyika usiku wa Alhamisi iliyopita.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye ni zao la kutoka kwenye akademia ya miamba hiyo ya Old Trafford hajaanzishwa kwenye mechi yoyote ya Ligi Kuu England tangu alipofanya hivyo kwenye mechi ya mwisho ya msimu uliopita huku jambo hilo likija ikiwa imepita miezi kadhaa tangu ilipomzuia kuondoka kwa mkopo kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mainoo alicheza dakika 171 katika ligi msimu huu na hii inatokana na kocha Amorim kuamua kuwatumia viungo wawili wenye uzoefu mkubwa, Bruno Fernandes na Casemiro katika eneo hilo la katikati ya uwanja.
Gwiji wa Man United, Paul Scholes amemshutumu kocha Amorim kwa kitendo hicho akisema Mainoo anapaswa kupewa nafasi ya kuanza kwenye mechi kama ilivyo kwa wachezaji wengine.
Katika posti yake kwenye mtandao wa Instagram, Scholes kwa hasira alisema Mainoo anaharibiwa kutokana na kunyimwa nafasi ya kucheza huku timu ikikosa nguvu ya kumiliki mchezo.
Mainoo, Tom Heaton, 39, kipa veterani ambaye ni chaguo la tatu, beki Tyrell Malacia na Lisandro Martinez, ambaye amerejea uwanjani akitokea kuuguza maumivu ya goti ni wachezaji pekee kwenye kikosi hicho cha Man United, ambao hawajapata nafasi ya kuanzishwa kwenye mechi ya Ligi Kuu England msimu huu.