Amorim apika tiba ya Rashford
Muktasari:
- Amorim amejiunga na United hivi karibuni akichukua nafasi ya Erik ten Hag ambaye alitimuliwa kwenye kikosi hicho baada ya kupata matokeo mabaya.
Manchester, England: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amemwambia staa wa timu hiyo, Marcus Rashford kuwa anatakiwa apambane kurudi kwenye ubora wake, lakini naye atamsaidia.
Amorim amejiunga na United hivi karibuni akichukua nafasi ya Erik ten Hag ambaye alitimuliwa kwenye kikosi hicho baada ya kupata matokeo mabaya.
Rashford alifunga bao katika sekunde ya 80 katika mchezo wa kwanza wa Amorim timu hiyo ilipovaana na Ipswich kwenye Uwanja wa Portman Road na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Hivi karibuni mshambuliaji huyo raia wa England hakuwa kwenye kiwango bora baada ya kuondolewa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa.
Akiwa chini ya Ten Hag, Rashford alifunga mabao 30 kwenye msimu wa kwanza wa bosi huyo lakini msimu uliopita alifunga mabao manane tu na msimu huu ana mabao manne.
“Nipo hapa kwa ajili ya kumsaidia kuwa bora,” alisema Amorim ambaye alimchezesha Rashford kama mshambuliaji wa mwisho kwenye mchezo uliopita.
“Nitajitahidi sana kuhakikisha anakuwa bora, siyo kwake tu hata kwa wachezaji wengine, lakini anatakiwa naye kujikubali kama Rashford, lazima arudi kwenye ubora wake aliokuwa nao miaka kadhaa iliyopita,” alisema kocha huyo.