Amad Diallo ampigia debe Michael Carrick kimtindo
Muktasari:
- Man United itakuwa ikilenga kuendeleza mwendelezo wao mzuri Jumatatu ijayo watakapokwenda Hill Dickinson kukipiga na Everton.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA wa Manchester United, Amad Diallo, amesisitiza umuhimu wa Michael Carrick kufuatia kuimarika kwa kiwango cha timu hiyo maarufu kama Mashetani Wekundu. Kiungo huyo wa zamani alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu baada ya kufutwa kazi kwa Ruben Amorim.
Carrick amesaini mkataba wa kuinoa timu hadi mwisho wa msimu huu, ingawa kumekuwa na wito wa kupewa kazi hiyo kwa dili la kudumu kufuatia matokeo mazuri ya ushindi mara nne na sare moja katika michezo mitano. Matokeo hayo yameifanya Man United kupanda hadi katika nafasi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Winga Amad sasa ametoa maoni yake kuhusu Carrick na kumpa sifa kubwa. Akizungumza kwenye podikasti ya Inside Carrington, amesema:
“Nadhani kuwa na Michael Carrick kama kocha mkuu ni jambo muhimu sana kwa sababu anaijua klabu. Yeye ndiye mtu sahihi wa kutuambia kuhusu klabu tunayochezea. Kabla ya mechi anatuambia: ninyi mnacheza kwa ajili yenu, lakini pia mnacheza kwa ajili ya mashabiki, na anasisitiza kwamba mashabiki ni muhimu sana kwetu.
“Sisi pia tunacheza kwa ajili ya mashabiki kwa sababu tunataka kushinda na tunataka kuwapa kitu kama shukrani. Kuwa na Carrick kunafurahisha sana na tunafurahia mazoezi. Ni mtu mzuri. Anaongea na kila mtu na nina bahati kwa sababu nilimkuta hapa nilipofika nikiwa na miaka 18. Pia niliwahi kucheza dhidi yake alipokuwa Championship, hivyo nimemfahamu kwa muda mrefu na ni mtu mzuri.”
Kwingineko, Amad pia amezungumzia kurejea kwa Jonny Evans, ambaye amerudi klabuni kama sehemu ya benchi la ufundi la Carrick. Mchezaji huyo kutoka Ivory Coast anaamini uzoefu na uelewa wake wa klabu ni wa thamani kubwa.
Aliongeza: “Ni muhimu sana kama mchezaji kuwa na watu karibu yako wanaoijua klabu na wanaojua maana halisi ya klabu hii kwao. Wanaendelea kutuambia inamaanisha nini, na hilo ni jambo muhimu sana. Na tunapoingia uwanjani tunataka kupigana kwa ajili yao. Hivyo ni muhimu kuwa na watu wa aina hiyo.”
Man United itakuwa ikilenga kuendeleza mwendelezo wao mzuri Jumatatu ijayo watakapokwenda Hill Dickinson kukipiga na Everton.