Al-Hilal yafanya kufuru kwa Nunez
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Liverpool na Al-Hilal tayari zimefikia makubaliano ya ada ya uhamisho na klabu hiyo ya Saudia italipa Pauni 46 milioni pamoja na nyongeza ya malipo ya baadaye (add-ons), ili kumsajili mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uruguay.
LIVERPOOL, ENGLAND: STAA wa Liverpool, Darwin Nunez imeripotiwa atapata mshahara marafudu iwapo atakamilisha uhamisho wake kwenda kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Al-Hilal.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Liverpool na Al-Hilal tayari zimefikia makubaliano ya ada ya uhamisho na klabu hiyo ya Saudia italipa Pauni 46 milioni pamoja na nyongeza ya malipo ya baadaye (add-ons), ili kumsajili mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uruguay.
Kiasi hicho cha pesa ni punguzo kubwa sana ukilinganisha na uhamisho wake wa awali kutoka Benfica kwenda Liverpool mwaka 2022, uliogharimu Pauni 85 milioni.
Kwa mujibu wa tovuti ya talkSPORT, Nunez atafaidika kifedha kwa kukubali kujiunga na Al-Hilal kwani atalipwa mshahara wa hadi Pauni 400,000 kwa wiki, kiasi ambacho ni takribani mara tatu ya mshahara wake wa sasa wa Pauni 140,000 kwa wiki akiwa Anfield.
Tetesi kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo zimekuwa zikisambaaa kwa muda mrefu tangu kuanza kwa mwaka huu.
Januari mwaka huu, Liverpool ilikataa ofa ya Al-Nassr, vilevile Napoli na AC Milan zilionyesha nia ya kutaka kumsajili lakini zilishindwa kutokana na bei kubwa waliyotajiwa.
Nunez alijiunga na Liverpool akitokea Benfica na kutajwa angeisaidia timu hiyo, lakini tofauti na matarajio, hakuendana na dau lililolipwa.
Tangu ajiunge, ameifungia Liverpool mabao 40 katika mechi 143, lakini amekuwa akikosolewa mara kwa mara kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi.
Msimu uliopita alifunga mabao saba tu na kutoa asisti nne katika mechi 45 alizocheza kwenye mashindano yote.
Nafasi yake pia imezidi kuwa ya mashaka hususani baada ya kusajiliwa Hugo Ekitike na tetesi zikidai majogoo hao wapo katika mpango wa kumshusha Alexander Isak kutoka Newcastle ambaye imefikia hatua nzuri katika mchakato wa usajili wake.