AJE ASIJE! Haaland akitua huku watatisha balaa England

Wednesday April 07 2021
Haaland pc

LONDON, ENGLAND. Wakala wa straika Erling Braut Haaland, Mino Raiola kwa sasa ni kama yupo ziarani kwenye nchi mbalimbali za Ulaya akijaribu kutafuta mteja sahihi wa kumnunua mteja wake kwa ajili ya msimu ujao.

Mkataba wa Haaland huko Borussia Dortmund unafichua kwamba huduma yake inaweza kupatikana kwa mkwanja usiozidi Pauni 70 milioni itakapofika mwakani kulingana na kipengele kilichochomekwa kwenye mkataba huo, lakini Raiola anatafuta soko kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kumuuza kwa faida.

Ripoti zinadai kwamba Raiola amelenga kupata Euro 20 milioni kama bonasi yake akimuuza staa huyo kwenye dirisha lijalo, huku akitaka pia mteja wake avute dili moto litakalomshuhudia akilipwa mshahara wa Euro 30 milioni kwa mwaka.

Hivi karibuni wakala huyo akiwa ameandana na baba yake straika Haaland walionekana huko Hispania, hasa Barcelona kwenda kuzungumza na mabosi wa timu hiyo ya Nou Camp ili wamsajili fowadi huyo wa zamani wa Molde na RB Salzburg.

Wameripotiwa kuzungumza pia na Real Madrid. Lakini, Barcelona wanahitaji zaidi huduma yake kwa sababu rais Joan Laporta anaamini saini yake inaweza kuwa ushawishi mkubwa wa Lionel Messi kusalia kikosini.

Ubora wa Haaland kwa msimu huu wa 2020/21, ambapo amefunga mabao 33 katika mechi 31 alizochezea Dortmund umezifanya timu nyingi kufukuzia saini yake, ikiwamo vigogo wa Ligi Kuu England ambao ni Manchester United, Manchester City, Chelsea na Liverpool.

Advertisement

Kukaba kwa uchumi huko Ulaya kutokana na janga la corona inaripotiwa kwamba jambo hilo linaweza kuzifanya klabu za Hispania kushindwa kummudu Haaland na kufanya vita hiyo ibaki kwa wababe wa Ligi Kuu England.

Kutokana hilo kumeibuka mjadala mwingine, kama Haaland atakwenda kujiunga na moja ya timu hizo za Ligi Kuu England ni wapi kutakuwa na kikosi matata kabisa kitakachotishia wapinzani uwanjani?

Pengine hili linaweza lisiwepo kwenye mawazo ya makocha wa timu hizo, Ole Gunnar Solskjaer, Thomas Tuchel, Pep Guardiola na Jurgen Klopp, lakini kunasa huduma ya Haaland kutazifanya baadhi ya timu kwenye orodha hiyo kuwa tishio zaidi kwa vikosi vyao vya uwanjani.

Wapi patakuwa tishio zaidi, Old Trafford, Stamford Bridge, Etihad au Anfield kwenye kucheza mechi wakati miamba yenye viwanja hivyo vitakapokwenda kunasa huduma ya mshambuliaji huyo ambaye bila ya shaka saini yake itakuwa ya gharama kubwa kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.


Manchester City (4-3-3)

Hakuna ubishi, kikosi hiki lazima kiondoke na ubingwa wa Ligi Kuu England, hakuna namna. Kwa sasa Man City inatafuta mrithi wa Sergio Aguero na ni jambo la wazi kabisa, Haaland ni mtu sahihi kwenda kuvaa buti za Muargentina huyo huko Etihad. Na hakika kama Haaland atanaswa na kocha Guardiola basi suala la kufunga mabao kwake halitakuwa tatizo kabisa kutokana na pasi za Kevin De Bruyne na mavitu ya Raheem Sterling, ambaye hana tofauti sana na kile ambacho Jadon Sancho amekuwa akifanya wanapokuwa pamoja kwenye kikosi cha Dortmund.


Chelsea (3-4-3)

Kwa namna fulani kwenye kikosi cha Chelsea, kocha Thomas Tuchel atakuwa na mtindo wa kipekee kabisa atakapofanikiwa kumnasa Haaland.

Tuchel ni mfuasi wa mfumo wa 3-4-3 na kwa kunasa huduma ya Haaland itamfanya kucheza fomesheni hiyo kwa uhakika mkubwa, ambapo kwenye safu ya washambuliaji wa tatu, atakuwa na Kai Havertz na Hakim Ziyech, ambaye watakuwa pembeni kwa pande zote mbili kulia na kushoto mwa Haaland.

Ujio wa Haaland kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge utawafanya Christian Pulisic na Timo Werner kuanzia kwenye benchi huko wakali kama Tammy Abraham na Olivier Giroud hawatakuwa na namna nyingine zaidi ya kutafuta tu timu za kwenda.


Liverpool (4-3-3)

Safu ya washambuliaji watatu waliopo tu kwa sasa kwenye kikosi cha Liverpool ni balaa zito na kama watafanikiwa kumnasa Haaland basi itakuwa shida zaidi kwa mabeki wa timu pinzani. Bila ya shaka Haaland akinaswa anakwenda kumwondoa Roberto Firmino kwenye kikosi cha kwanza na hivyo, ataunda utatu matata na wakali wawili wa Kiafrika, Mohamed Salah na Sadio Mane.

Kwa soka la Klopp, ambaye amekuwa muumini mkubwa wa kushambulia muda wote, akinasa huduma ya Haaland basi suala la Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England na pengine cha Ulaya kitakwenda wapi basi bila ya shaka kitatua Anfield.

Timu hii ya Liverpool yenye huduma ya Haaland bila ya shaka itakuwa na uwezo wa kutikisa pia hadi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kusaka ubingwa.


Manchester United (4-2-3-1)

Tatizo linalowakabili Manchester United kwa sasa linadaiwa kuwa ni mfungaji wa mabao. Miamba hiyo ya Old Trafford inapoteza nafasi nyingi sana za kufunga kutokana na mastraika wake kushindwa kufanya mambo ya maana kwenye timu. Wakati Paul Pogba kukiwa hakuna uhakika kama atabaki au vipi, huku miamba hiyo inayonolewa na Solskjaer ikitaka kumnasa Sancho, ujio wa Haaland utaweka mambo mengi tofauti hasa kwenye eneo lao la kushambulia ambalo limekuwa likipoteza nafasi nyingi. Kama Haaland atajiunga huko Old Trafford, basi moja kwa moja atakwenda kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, ambapo pembeni kushoto na kulia kutakuwa na Marcus Rashford na Anthony Martial huku nyuma yao kwenye Namba 10 kutakuwa na fundi wa mpira na pasi kali za mwisho, Bruno Fernandes.


Mambo ya kuzingatia

Kwa jinsi ilivyo, Haaland atakuwa na machaguo manne kwenye meza yake kwa sasa kabla ya dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi kufunguliwa mwisho wa msimu huu na bila ya shaka wakala wake, Raiola atakuwa bize kutafuta mahali patakapokuwa sahihi zaidi kwa mteja wake bila ya kuzingatia pesa zaidi kama kipaumbele.

Licha ya kwamba kila klabu ina mfumo wake tofauti ili kumfanya Haaland kufiti kwenye vikosi vyao, hakuna ubishi kwamba Man City na pengine Chelsea ndiko mahali panapomfaaa zaidi mshindi huyo ajaye wa Ballon d’Or. Hata hivyo, timu zote zimekuwa na ubora wa kutosha na uwezo wa kumpa Haaland nafasi ya kutamba kwenye Ligi Kuu England, licha ya kwamba dili za timu hizo zote zinaweza kutibuliwa na vigogo wa Hispania, Barcelona na Real Madrid ambazo kila mchezaji kwenye dunia hii atapenda kwenye kucheza kwenye timu hizo mbili za kibabe kabisa kwenye soka la Ulaya.

Advertisement