Aguero anatua Barca kiulaini

Thursday January 14 2021
pic aguero

Barcelona, Hispania. KITENDO cha Sergio Aguero kutosaini mkataba mpya na Manchesetr City hadi sasa kimeonekana kuwakosha Barcelona ambao, sasa wanajipanga kumsajili mshambuliaji huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 32.

Mkataba wa Aguero na Manchester City umebakiza muda wa miezi sita na mshambuliaji huyo kwa sasa yuko huru kufanya majadiliano na hata kusaini mkataba wa awali na klabu nyingine.

Klabu yake Manchester City bado inaonekana haijafikia uamuzi kama itamuongezea mkataba Aguero au itamuonyesha mlango wa kutokea jambo ambalo linaonekana kuzitamanisha timu mbalimbali ambazo zimeanza kuwania saini ya mshambuliaji huyo.

Miongoni mwa timu hizo ni Barcelona ambayo inamtaka Aguero kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji ambayo imekosa mshambuliaji wa asili wa kati tangu walipoachana na Luis Suarez katika dirisha la kiangazi huku pia kinda wake Ansu Fati akiwa anauguza majeraha ya goti aliyoyapata mwezi Novemba.

Barcelona inatajwa kutaka kuutumia uhusiano wa karibu uliopo baina ya nahodha wake, Lionel Messi na Aguero kama chambo ya kumnasa mshambuliaji huyo wa Manchester City ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha kwanza kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

Kiu hiyo ya Barcelona kwa Aguero imekuja siku chache baada ya PSG nayo kuonesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akimvutia kocha wao, Mauricio Pochettino aliyewahi kuinoa Tottenham Hotspur.

Advertisement

Hata hivyo, wakati Barcelona wakiingiia kupigana vikumbo na PSG kumuwania Aguero, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amekuwa akisisitiza kuwa bado wana mpango wa kuendelea kubaki na mshambuliaji huyo kikosini.

“Tunajua anamaanisha nini kwetu. Tunajua ni kwa jinsi gani tunamthamini ila anatakiwa kutuonyesha kila mmoja wetu wa kwanza nikiwa mimi kwamba tunatakiwa kuendelea kuwepo hapa, kucheza vizuri na kushinda mechi.

Baada ya hapo, klabu pamoja na mimi tunatakiwa kuamua kuhusu ubora wake. Pindi akicheza katika kiwango hatuna shaka ni mchezaji anayetakiwa kubakia hadi pale atakapoamua kuondoka. Ni mchezaji wa kipekee. Ni muhimu kwetu, kwa mashabiki na kwa kila mmoja,” alisema Guardiola.

Advertisement