Afif nyie acheni tu

NYOTA mwenye asili ya Tanzania, Akram Afif alikuwa shujaa wa Qatar wakati nchi hiyo ilipotwaa taji lake la pili mfululizo la AFC Asian Cup dhidi ya Jordan Jumamosi.

Afif mwenye umri wa miaka 27, anayechezea klabu ya Al Sadd inayoshiriki Ligi Kuu ya Qatar, alipachika mabao matatu ‘hat trick’ katika ushindi wa 3-1 kwenye Uwanja wa Lusail, Qatar.

Alimaliza akiwa mfungaji bora wa michuano hiyo akiwa amefunga mabao nane.

Tumeona aina nyingi za ushangiliaji mabao kwenye soka, lakini hii ilikuwa kiboko, baada ya kumzidi maarifa kipa wa Jordan Yazeed Abu Laila na kuweka kambani bao lake la kwanza kwenye mchezo huo.

Afif alianza kukimbia hadi kwenye kona, akasimama na kutoa kadi ambayo ilikuwa na neno ‘S’, mara baada ya mchezo nyota huyo alieleza alifanya hivyo kwa ajili ya heshima kwa mke wake.

“S ndio herufi ya kwanza ya jina la mke wangu,” alisema. “Ilikuwa mara yake ya kwanza kuwa uwanjani.”

Afif ambaye viongozi wa Simba na Yanga waliwahi kumtembelea huko Qatar na kumpa zawadi ya jezi za timu zao,  alizaliwa Doha, baba yake ni Msomali, Hassan Afif kutoka kabila la Yafa, na mama yake Afif anatoka Yemen.

Uasili wake na Tanzania, unakujaje? Babake Afif alizaliwa Tanzania kabla ya kuhamia Somalia.