Aaliyah katika ndoto za Ramos kumpata Pilar

Muktasari:
- Nje ya soka alikuwa na ndoto nyingine iliyomtokea mara tatu nayo ni kuwa na mwanamke mwenye mvuto zaidi duniani, Pilar Rubio, 47, na hilo alilifanikisha kama alivyoshinda mataji matano ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa.
Misimu 16 ilimtosha Sergio Ramos, 39, kuitumikia Real Madrid akiwa beki wa kati. Ndoto nyingi kama mchezaji amezitimiza hapa, Santiago Bernabeu ilimpa kila kitu akishinda mataji yote ngazi ya klabu tena kwa zaidi ya mara moja.
Nje ya soka alikuwa na ndoto nyingine iliyomtokea mara tatu nayo ni kuwa na mwanamke mwenye mvuto zaidi duniani, Pilar Rubio, 47, na hilo alilifanikisha kama alivyoshinda mataji matano ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa.
Licha ya tofauti yao ya umri, yaani miaka minane, haikuwa kikwazo kwake. Ni kama alivyoimba msanii kutoka Marekani, Aaliyah katika wimbo wake, Age Ain’t Nothing but a Number (1994) akiwa na maana umri sio kitu ila ni namba tu.
Ikumbukwe Aaliyah aliyefariki dunia Agosti 25, 2001 katika ajali ya ndege huko Bahamas, alitoa wimbo huo chini ya Blackground Records na Jive Records akiwa na umri wa miaka 15 na hadi sasa ni moja ya nyimbo zake zinazouza zaidi.
Uhusiano wa Ramos na Pilar ulianza Septemba 2012 na kwa mara ya kwanza kuonekana pamoja ni katika hafla ya tuzo za Ballon d’Or ya mwaka huo na tayari wana watoto wanne na wote wa kiume kuna Sergio Jr, Marco, Alejandro na Maximo Adriano. Mnamo Julai 16, 2018 Ramos na Pilar walichumbiana kisha mwaka mmoja baadaye, yaani Juni 15, 2019 wakafunga ndoa huko Sevilla, moja ya miji mikubwa zaidi Hispania.
Pilar ni mtangazaji maarufu wa televisheni na mwanamitindo huko Hispania akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 11 katika ukurasa wake wa Instagram - mtandao aliojiunga nao Oktoba 2014.

Katika televisheni ameonekana kwenye matangazo ya Amstel, Canal+ na Hyundai, lakini mafanikio yaliyomtambulisha kwa watu wengi yalikuja baada ya kuonekana katika kipindi cha vichekesho cha La Sexta na aliripoti makala mbalimbali za habari. Alishinda tuzo ya Mtangazaji Bora wa Televisheni kutoka Premio Joven 2007, huku kati ya 2008 na 2009 akitajwa kama mwanamke mwenye mvuto zaidi duniani katika jarida la FHM, toleo la Hispania.
Septemba 2019, Ramos katika ‘documentary’ yake ‘The Heart of Sergio Ramos’ iliyoruka Amazon Prime, alifunguka jinsi alivyokutana na Pilar na kudai kuwa alishamuota mara tatu mtangazaji huyo, hivyo ilikuwa ndoto yake kuwa naye. “Ilikuwa ni jambo lisilo la kawaida kuota ndoto mara tatu kuhusu mtu yuleyule. Na ni kweli nilimfahamu kwa sababu alikuwa mtangazaji wa televisheni,” anasema Ramos
“Hatukuwa na kitu chochote cha kutuunganisha au kufafana ila niliamua kujaribu kutupa kete, kuna sauti ilikuwa ikinisisitiza jaribu kufanya jambo ingawa sikuwa na matarajio mengi ya kupata majibu.”
“Lakini kwa jinsi muda ulivyokuwa unakwenda ilionekana mkakati ulianza kufanya kazi ipasavyo na kuanzia hapo tukafahamiana kwa kiwango kikubwa kama ilivyo hii leo.”
Hata hivyo, wakati wakiendelea kufanya siri ya jinsi walivyokutana kwa mara ya kwanza, harusi yao ilikuwa ya aina yake ikihudhuriwa na wachezaji wenzake wakati huo na waliowahi kupita Real Madrid kama Marcelo, Jordi Alba na David Beckham.

Kufuatia usajili wake wa kushtua, Februari, mwaka huu mtandao wa Daily Mail uliripoti Pilar amekataa kuhamia Mexico ambapo Ramos amesajiliwa na Monterrey inayoshiriki Ligi Kuu (Liga MX).
Pilar alisema alishahama mara mbili akimfuata Ramos katika kazi yake ya soka, lakini sasa imetosha na ukizingatia kahamia mbali yaani kutoka Ulaya hadi Amerika Kuskazini - bara alikozaliwa Aaliyah.
Piar alifanya hivyo Ramos alipojiunga na Sevilla na Paris Saint-Germain (PSG) akitokea jiji la nyumbani kwao, la Madrid, lakini sasa hataki tena kuhama bali atabaki nyumbani na familia huku akiendelea na kazi yake ya utangazaji.
Mwandishi na YouTuber, Javi de Hoyos ananukuu chanzo cha karibu na Pilar kikieleza mrembo hiyo amechoka kuzungushwa huku na kule miaka ya karibuni mara Sevilla, Paris na sasa Mexico!.
“Sababu za kikazi ndizo zilizomrudisha Madrid na ndipo anataka kukaa, bila kujali suala la Monterrey. Pilar ana miradi mingi ijayo kama vipindi vya televisheni vya El Desafio na Maestros de la Costura, hivyo hatahamia Mexico na Ramos,” anasema.

“Ijumaa iliyopita, mtu wa karibu wa Pilar aliniambia alikuwa amechoka kuhama. Alikwenda naye Paris kisha Ramos akaenda Seville. Baadaye aliamua kwenda Madrid kwa sababu za kikazi. Anapenda sana kuishi huko.”
Wakati Ramos anafanya uamuzi huu, Pilar anasema: “Safari hii sitakubali. Tayari nimehama mara mbili. Sasa nakaa hapa Madrid. Familia inakaa hapa. Familia inakaa hapa. Ramos nenda peke yako hatuwezi kuhama tena,” Javi alinukuu chanzo hicho.
Ikumbukwe Ramos amechezea klabu kadhaa, lakini Real Madrid ndipo alipodumu kipindi kirefu kuanzia 2005 hadi 2021, na kwa kipindi chote akiwa na wababe hao wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) alicheza michezo 469 na kufunga mabao 72.