Umakini wa kipa Neuer wampagawisha Guardiola
Lahm Neuer
Muktasari:
Jioni moja akipata mlo wa jioni Allianz Arena, Pep aliungana nasi kuangalia video moja isiyo ya kawaida ambayo ilirekodiwa kutoka jukwaa kuu, ilikuwa ikimmulika kipa Neuer pekee wakati Bayern ikishambulia kwenye goli la timu pinzani.
TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi, Marti Perarnau aliyachambua mafanikio ambayo Pep Guardiola, alianza kuyapata kwa wachezaji kucheza alivyowaelekeza hadi kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Bremen huku Franck Ribery akiimudu vyema namba 9 feki. Sasa endelea…
Mechi hiyo kwa Pep ilikuwa ni rekodi ya kushinda mechi ya 200 katika mechi rasmi 274 katika timu za Barcelona pamoja na Bayern. Akiwa kocha wa Bayern pia alikuwa amejiwekea rekodi kwenye Bundesliga kwa kutofungwa katika mechi zake 15 za awali. (Rekodi ambayo aliendelea kuiboresha).
Pia kulikuwa na habari nyingine nzuri kwa Pep, Bayern Leverkusen iliichapa Borussia Dortmund bao 1-0, matokeo hayo maana yake ni kwamba Bayern ilikuwa mbele kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya mahasimu wao Dortmund. Bayern walikuwa mbingu ya tisa.
Kilichokuwa kikisubiriwa hapo ni mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ili kuona kocha Manuel Pellegrini (enzi hizo akiwa City) alikuwa ameiandaa vipi timu yake.
“Wakati yote hayo yakitokea, Dortmund ilikuwa ikinolewa na Jurgen Klopp ambaye kwa sasa anainoa Liverpool kama ambavyo Pep sasa ni kocha wa Man City).
Pamoja na hali hiyo, bado Pep alichukizwa na makosa yaliyofanywa uwanjani, lakini alikuwa tayari kuwasamehe wachezaji ingawa kwa kumwangalia kuwa mwenye hasira lakini kwa watu wake wa ndani wanajua hali halisi aliyokuwa nayo.
Anakubali ukweli kwamba makosa huwa yanatokea, hata yeye alikuwa mchezaji na enzi zake alikuwa akifanya makosa ingawa huwa anakerwa pale na mchezaji anaposhuka kiwango cha sababu tu anaamini ana kila kitu.
Pep anashikamana na imani kwamba katika michezo unatakiwa kushinda kila kitu na hilo linatokana na juhudi za kila siku pamoja na umakini, na ndio maana haishangazwi kwa namna ambavyo anavutiwa na wanasoka kina Mascherano na Iniesta wa Barcelona pamoja na Lahm na Neuer wa Bayern, kati ya wachezaji hao hakuna anayepoteza umakini katika mechi. Ni wapiganaji wa wakati wote.
Jioni moja akipata mlo wa jioni Allianz Arena, Pep aliungana nasi kuangalia video moja isiyo ya kawaida ambayo ilirekodiwa kutoka jukwaa kuu, ilikuwa ikimmulika kipa Neuer pekee wakati Bayern ikishambulia kwenye goli la timu pinzani.
Katika video hiyo, unaweza kumuona Neuer akisogea na kujaribu kutoa maelekezo mafupi kwa Dante na Boateng na hiyo ni kwa sababu walichokuwa wakifanya Bayern ni kujihakikishia umiliki wa mchezo mwanzo mwisho.
Timu pinzani ilikuwa umebanwa katika eneo lao lakini Neuer alikuwa akifuatilia kila hatua ilikuwa kama vile alikuwa karibu na tukio lakini ukweli ni kwamba alikuwa golini kwake, umbali wa kama mita 60 hivi au zaidi.
Hajawahi kupoteza umakini wakati akizunguka katika eneo lake na hata nje ya eneo lake huku akiwa pamoja na timu huku akifuatilia wapi kwenye mapungufu katika mfumo wa timu nzima ya Bayern ili aweze kuingilia na kuweka mambo sawa.
Pep aliguswa na video hiyo na akaishia kusema, “Neuer ni wa kipekee, ni hivyo tu.”
Ni kama vile walikuwa wamechagizwa na mafuriko ya Bremen, Bayern walijitupa kamili kuikabili City kwenye Uwanja wa Allianz Arena, kwa mara nyingine Ribery alikuwa akicheza namba 9 feki wakati Mandzukic aliruhusiwa kushuka kidogo kama ambavyo mwenyewe alitaka na Muller alitupwa winga ya kulia.
Itaendelea Jumamosi ijayo…