Tuchel amnyooshea kidole Lukaku

He! Lukaku kurudi Italia

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Chelsea, Thomas Tuchel, amemtolea uvivu, Romelu Lukaku baada ya kushindwa kuisaidia timu kuepuka kipigo cha bao 1-0, lililofungwa na Kevin de Bruyne walichopata dhidi ya Manchester City juzi kwenye Uwanja wa Etihad.

Tuchel amechukizwa na namna Lukaku alivyokosa nafasi adimu aliyopata eneo la hatari la Man City kipindi cha kwanza cha mtanange huo.

Katika mechi hiyo Chelsea ilipiga shuti moja tu ambalo lililenga lango dhidi ya Man City huku Tuchel akimtupia lawama Lukaku kwa kushindwa kufunga bao.

Lukaku aliwekwa benchi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool mwezi uliopita kutokana na sintofahamu iliyotokea baada ya kutamka wazi kuwa hana furaha chini ya Tuchel, kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports Italia.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, Tuchel alisema umakini ulisababisha kupokea kichapo hicho na kuipa Man City mwanga mzuri kuelekea ubingwa wa msimu huku wakiwa wamepitwa pointi 18.

“Lukaku amepoteza mipira kizembe bila ya presha yoyote, bila shaka Lukaku alipata nafasi nyingi ameshindwa kuzitumia, ni mchezaji wetu tunamthamini lakini anatakiwa na yeye aonyeshe kitu, kiukweli amezingua sana,” alisema Tuchel.

Tangu Lukaku alipotua Stamford Bridge kwa kitita cha Pauni 98 milioni amekuwa na wakati mgumu na tetesi za usajili zimeripoti huenda akatimka huku PSG ikionyesha kila dalili ya kumhitaji straika huyo wa kimataifa wa Ubelgiji.