Liverpool presha tupu

Saturday January 16 2021
liverpool pic

LIVERPOOL, ENGLAND. HATIMA ya Liverpool kutwaa taji au kuondoka patupu msimu huu itaamuliwa ndani ya kipindi cha siku 34 zijazo kutokana na ugumu wa ratiba watakayokabiliana nayo ndani ya muda huo.

Mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu ya England, watalazimika kucheza mechi 10 ndani ya siku 34 ukiwa ni wastani wa siku 3 tu kutoka mchezo mmoja hadi mwingine jambo linaloweza kuwaweka katika uwezekano finyu wa kutetea taji ubingwa na kufanya vyema katika Kombe la FA.

Timu hiyo imekuwa na mwendo wa kusuasua katika siku za hivi karibuni baada ya kupata sare mbili dhidi ya vibonde, Newcastle na West Brom na mbaya zaidi wakapoteza mbele ya Southampton jambo lililowafanya wapoteze uongozi wa msimamo wa Ligi Kuu England.

liverpool pic 1

Kipindi hicho kigumu kwa Liverpool kitaanzia Jumapili mwishoni mwa wiki hii ambapo watwaalika vinara wa ligi, Manchester United ambao wako mbele yao kwa tofauti ya pointi tatu na ikiwa watapoteza, ambao wanalazimika kupata ushindi ili kurudi kilele mwa msimamo wa ligi.

Lakini baada ya mechi hiyo, Liverpool italazimika kukabiliana na United, siku sita baadaye katika mechi ya hatua ya 32 bora ya Kombe la FA na kisha baada ya hapo watakuwa na mchezo mgumu ugenini dhidi ya Tottenham ya Jose Mourinho.

Advertisement

Baada ya hapo, Liverpool itarudi nyumbani kuikabili West Ham kisha mechi zinazofuata watacheza dhidi ya Brighton, Manchester City, Leicester na Everton

liverpool pic 2

Ikumbukwe kuwa Liverpool itacheza mechi hizo 10 huku ikiendelea kuwakosa nyota wake muhimu wanaocheza nafasi ya beki wa kati, Virgil va Dijk na Joe Gomez ambao wanauguza majeraha kwa muda mrefu sasa hali iliyopelekea kocha Jurgen Klopp kuwatumia baadhi ya viungo wake kucheza katika nafasi hiyo.

Mbali na changamoto hiyo ya majeraha, Klopp pia anatakiwa kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa salama dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Covid 19 ambayo yanaweza kupelekea awakose nyota wake muhimu katika baadhi ya mechi kama ambavyo iliwahi kutokea kwa mshambuliaji wake, Sadio Mane.

Advertisement