Lampard akiri presha itamfukuzisha Chelsea

LONDON, ENGLAND. IMEKUWA ni kipindi kigumu kwa Frank Lampard. Pengine anakumbuka nyakati za furaha alizowahi kuwa nazo kwenye viunga hivyo wakati anahudumu kama kiungo mtiifu.

Atafanya hivyo ili kujiliwaza, kwani yeye mwenyewe amethibitisha kwamba kibarua chake kipo kwenye mstari mwekundu ikiwa matokeo mabaya yataendelea kutawala kwenye ubao wa Stamford Bridge.

Lampard ambaye ameshuhudia kikosi chake kikicheza mechi tatu mfululizo bila ya kupata ushindi yupo kwenye presha kubwa ya kupoteza kibarua chake na makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kuchukuwa mikoba yake ni Ralph Hassenhuttl, Julian Nagelsmann na Thomas Tuchel.

Taarifa zinadai mabosi wa Chelsea wamempa mchezo mmoja ambao ni dhidi ya Fulham, Ijumaa ya wiki hii, ikiwa atapoteza basi ndio itakuwa safari yake. Mechi yao ya jana ya Kombe la FA dhidi ya timu ya Daraja la Nne ya Morecambe haimo katika vipimo vyake.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa wababe hao Marina Granovskaia ameonyesha kumsapoti zaidi kocha huyo na kumlinda katika kipindi hiki kigumu.

Ikumbukwe Lampard alifanya vizuri sana wakati anapewa timu Julai 4, 2019 ikiwa kwenye katazo la kusajili na akaamua kuuchukuwa mzigo huo wa kuni zenye miba bila ya kujali kuchomwa hadi akaiongoza kumaliza nafasi ya nne.

“Jambo pekee ninalohitaji kufanya kwa wakati huu ni kufikiria jinsi gani timu inaweza kupata matokeo mazuri na siwezi kuangalia mambo mengine ambayo yanatokea tofauti na kazi yangu kwa sababu itakuwa inanipotezea muda bure,’’ alisema Lampard na kuongeza:

“Mwezi mmoja uliopita kila kitu kilikuwa sawa lakini mwezi huu mambo yamebadilika kwa haraka na kila mtu anaongea jambo baya kuhusu sisi.

“Nilihisi amani sana pale nilipopokewa kwa mara ya kwanza baada ya kurejea kuifundisha timu hii na ilikuwa hivyo hata wakati nahudumu kama mchezaji katika kipindi cha miaka 13 nilichokaa, niliondoka kwa sababu walihitaji kuwa na damu mpya kwenye kikosi.

“Kwa muda huu naelewa jinsi mpira ulivyo kuanzia mahitaji na matarajio, hivyo sidhani kama naweza kuwa na uwezo wa kubakia ikiwa kuna sababu za kuniondoa, jambo ninaloweza kusema kwa sasa najaribu kuwa wazi kwa hali inayoendelea na hatma yangu ni mambo yanayoonekana kurandana.”

Lampard anasisitiza kwamba ili aendelee kusalia kwenye viunga hivyo ni lazima wachezaji wake wabadilike na kurudi kwenye mstari la sivyo ni ngumu sana yeye kuendelea kuhudumu.

“Najua sababu kubwa ni kwamba nina wachezaji wengi vijana ambao walijitoa sana msimu uliopita na msimu huu pia nina wachezaji wapya ambao wameingia kwenye kikosi ambao unategemea waende kwenye ligi kama EPL na wakupe matokeo mazuri kwa haraka hilo ni jambo gumu sana na lipo nje ya uwezo wangu kwa sababu nimetengeneza mfumo na kuwaelekeza namna ya kucheza, zaidi ya hapo ni wachezaji wenyewe ndio wanatakiwa waonyeshe walichonacho,” alisema.

Hata hivyo, Lampard alisema suala la yeye kuondoka ama kubaki lipo mikononi mwa mmiliki wa timu hiyo bilionea Roman Abramovich.

Vile vile akaongeza kwamba kazi aliyofanya msimu uliopita kuiwezesha timu kumaliza nafasi ya nne ni moja kati ya mambo yanayosababisha hadi sasa awepo kwenye timu hiyo.

“Kabla ya msimu kuanza nilijua hili litakwenda kutokea, kwa sababu nilikuwa na wachezaji wengi ambao hawana ukomavu wa kutosha na sikupata nafasi ya kukaa nao kwa muda mrefu, nakumbuka wakati mimi nasajiliwa nikiwa kijana mdogo mwaka wa kwanza nilikuwa mchezaji wa kawaida mwaka wa pili kiwango kikaongezeka, mwaka wa tatu kikawa mara dufu na mwaka wanne ndio kikawa bora zaidi na hili ndio naliona kwa wachezaji wapya lakini siwezi kumuaminisha kila mtu kile ninachoamini,” alisema.