Klopp atibua hali ya hewa

Klopp atibua hali ya hewa

LIVERPOOL, ENGLAND. KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) hayana ukubwa wowote, kauli ambayo imemuweka kwenye kiti moto.

Klopp alitoa kauli hiyo iliyowakera watu baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0, ilipomenyana na FC Porto kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, usiku wa kuamkia jana.

Kocha huyo ametakiwa kuomba radhi kutokana na kauli hiyo tata aliyoitoa wakati wa mahojiano kuhusu mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ilipomalizika.

Liverpool itawakosa mastaa wake Sadio Mane na Mohamed Salah ambao wataungana na timu zao za taifa, kushiriki michuano ya Afcon itayoanza Januari, mwakani nchini Cameroon. Ndani ya chumba hicho cha habari alisikika ripota mmoja akimuumbua Klopp akidai kauli hiyo ni tusi kwa mastaa hao kutoka Afrika, hivyo akimtaka kuomba radhi.

“Nadhani umewadhihaki wachezaji wako na watu wa bara la Afrika kiujumla, haikuwa sahihi kusema kauli kama hiyo, nadhani unatakiwa kuomba radhi bara zima la Afrika kutokana na kauli hiyo,” alisema mwanahabari huyo.

Hata hivyo, Klopp alijeteta na kusema watu wamemtafsiri vibaya baada ya kusema kauli hiyo.

“Sikumaanisha kusema hivyo nadhani hamkunielewa vizuri, sijui kwanini mmelewa hivyo kama ulivyosema hakika sifahamu kwanini, sikumaanisha kama michuano midogo naomba mnielewe hivyo,” alisema Klopp.