Kane aje Chelsea, Lukaku aende Spurs

Kane aje Chelsea, Lukaku aende Spurs

LONDON ENGLAND. CHELSEA inapiga mpango wa kumchukua Harry Kane na huenda ikamjumuisha Romelu Lukaku kubadilishana wachezaji na Tottenham Hotspur, imeripotiwa.

Kocha mpya wa The Blues, Graham Potter ni shabiki mkubwa wa straika huyo wa Spurs. Hivyo, Chelsea inaweza kukoleza mwendo wa kumsajili Kane wakati Lukaku atakaporejea Stamford Bridge kutoka Inter Milan, anakocheza kwa mkopo kwa sasa.

Chelsea wao wanataka wawape Spurs pesa pamoja na Lukaku ili tu wamchukue Kane, kwa mujibu wa ripoti ya Calciomercato.

Lakini, Lukaku anaonekana kuwa na furaha Inter Milan na Chelsea ilikuwa na makubaliano na klabu hiyo ya Italia kwamba inaweza kuendelea kubaki na straika huyo wa Ubelgiji kwa mkopo kwa mwaka wa pili huko San Siro.

Gwiji wa masuala la uhamisho wa wachezaji, Gianluca Di Marzio aliripotiwa mkopo wa pili unaweza kuwagharimu Inter Pauni 9 milioni, licha ya kuwapo na makubaliano pia ya kumchukua jumla kama watanogewa zaidi.

Lukaku ameweka wazi mapenzi yake na Inter na atakuwa tayari kubaki, licha ya kujiunga na Spurs kutampa nafasi ya kwenda kukutana na kocha Antonio Conte. Shida inaweza kuwa Kane, haonekani kuwa na uwezekano wa kwenda Stamford Bridge kutokana na upinzani wa Chelsea na Spurs. Staa huyo Mwingereza kwa siku za karibuni amekuwa akihusishwa na Bayern Munich.