Henry aipigia saluti Liverpool

Henry aipigia saluti Liverpool

LONDON, ENGLAND. MKONGWE wa soka Thierry Henry na nyota wa zamani wa Arsenal, ameukubali mziki wa Liverpool huku akisisitiza kiwango walichoonyesha msimu huu ni moto wa kuotea mbali huku akitoa onyo kwa timu pinzani.

Henry alisema hayo baada ya Liverpool kuibamiza Everton mabao 4-1 katika mchezo wa derby uliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Katika mchezo huo nyota wa Liverpool, Mohamed Salah alicheka na nyavu mara mbili, mengine yakiwekwa kimiani na Jordan Henderson na Diogo Jota huku Everton ikiweka rekodi ya kufungwa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu miaka 39 iliyopita.

Licha ya kipigo hicho cha Everton kwa mara ya kwanza, Henry alisifu kiwango cha Liverpool huku ushindi huo ukiwapa presha zaidi Chelsea na Manchester City, kuelekea mbio za ubingwa msimu huu.

“Kwa upande wangu, Liverpool ipo sayari nyingine kwa sasa, sio tu wao hata wapinzani wao (Chelsea na Man City) wapo kwa kiwango cha juu sana, Liverpool imetoka kuifunga Arsenal mabao manne na Southampton mfululizo, unaweza kuitazama Liverpool kwa jicho la tofauti sana,” alisema Henry.

Liverpool itacheza mechi nyingine ya Ligi Kuu England ugenini kesho dhidi ya Wolves na vijana wa Jurgen Klopp wataingia uwanjani wakijiamini hasa kutokana na matokeo yao mazuri waliyopata mechi tatu mfululizo wakipasua watu ‘4-4-4.