Chilwell kupasuliwa mguu

LONDON, ENGLAND. BEKI wa Chelsea, Ben Chilwell huenda akafanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu baada ya kuumia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus usiku wa Jumatano.
Hata hivyo, Chelsea itasubiri majibu ya daktari Chiwell baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jeraha hilo kabla ya uamuzi kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa, Chelsea itasikilizia maendeleo ya Chilwell kama kuna ulazima wa beki wa kimataifa England, kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu.
Chilwell alishindwa kumaliza mchezo huo na kulazimika kutolewa nje ya uwanja akiwa anachechemea, Chelsea ikitoka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Juventus.
Kwa mujibu wa ripoti Chilwell aliumia vibaya na anaweza kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita hadi nane, hivyo ni pigo kubwa kwa Thomas Tuchel kumkosa nyota huyo wa Kimataifa wa England.
Kocha wa England, Gareth Southgate amejawa na hofu baada ya Chilwell kuumia hasa ukizingatia anamtegea beki huyo kuelekea kwenye fainali za Kombe la Dunia zitazofanyika Qatar mwakani.
Chilwell ana kiwango bora tangu alipopewa nafasi na kocha Tuchel akichukua nafasi ya Marcos Alonso kikosini Chelsea tangu msimu huu ulipoanza.