Casemiro alikuwa kama ana miaka 45

Manchester, England. Gabriel Agbonlahor amesema Casemiro anaonekana kuwa kama mwenye miaka 45 uwanjani, wakati Manchester United ilipochakazwa na Brighton.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil alikuwa miongoni mwa nyota waliocheza chini ya kiwango, wakati Man United ikilala kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Hicho ni kipigo cha tatu kwa kocha Erik ten Hag kwenye mechi tano za kwanza za msimu mpya wa Ligi Kuu England, wakati klabu hiyo ikiwa na matatizo ndani na nje ya uwanja.

Nyota huyo wa zamani wa England, Agbonlahor, akizungumza na talkSPORT, alishindwa kuilaumu Man United kutokana na mabao ya Danny Welbeck, Pascal Gross na Joao Pedro yaliyoipa ushindi Brighton, ukiwa ni wa nne mfululizo dhidi ya Man United.

Pia, alishindwa kuelewa kwanini Harry Maguire hakuanza badala ya Lisandro Martinez na Victor Lindelof waliokuwa na siku mbaya uwanjani.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Agbonlahor, Kocha wa Brighton, Roberto De Zerbi alisema ushindi wa vijana wake dhidi ya Manchester United haushangazi, kwani ameshaifunga miamba hiyo mara nne mfululizo.

Alipoulizwa kwanini Brighton imekuwa ikipata ushindi mbele ya Man United, De Zerbi alisema: "Mchezo wa soka ni mzuri kwa sababu timu ndogo inaweza kushinda muda wowote. Nadhani Brighton haijakuwa kubwa, lakini haishangazi tena kuifunga Man United.

"Ubora wa wachezaji na jinsi tulivyojiandaa ndani ya Brighton ni kitu cha msingi. Sijui tatizo la Manchester United, lakini naweza kuielezea timu yangu.

"Tunafanyia mazoezi mtindo wetu wa uchezaji, tunacheza kwa ari, tulikaba mtu kwa mtu ndani ya Old Trafford kwa muda wote na tulicheza mpira katrika eneo lote la uwanja.

"Kipindi cha kwanza, tulikuwa na wakati mgumu kutokana na presha, lakini baada ya hapo tulicheza soka safi."

Dalili nyingine ya msimu bora kwa Brighton itakuwa katika mashindano ya kwanza ya Ulaya kwa klabu hiyo, wakati itakapoivaa AEK Athens kwenye mechi ya Ligi ya Europa, Alhamisi.