"Bruno aachwe" Amorim awajia juu wachambuzi wa Man United

Muktasari:
- Nahodha wa zamani wa Man United, Roy Keane ni miongoni mwa wachezaji hao wa zamani ambao wamekuwa wakimkosoa sana Fernandes akisema si mpambanaji licha ya kuwa na kipaji kikubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Ruben Amorim amesema Bruno Fernandes ndio dhahabu ya Manchester United kwa sasa — hivyo amewataka mastaa wa zamani wa timu hiyo ambao kwa sasa ni wachambuzi wampumzishe na waache kumfuatafuata kiungo wake.
Nahodha wa zamani wa Man United, Roy Keane ni miongoni mwa wachezaji hao wa zamani ambao wamekuwa wakimkosoa sana Fernandes akisema si mpambanaji licha ya kuwa na kipaji kikubwa.
Hata hivyo, Fernandes, 30, amekuwa tumaini kubwa la Man United inayojitafuta na Alhamisi iliyopita alifunga hat-trick dhidi ya Real Sociedad kuisaidia timu hiyo kufuzu hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Europa League.
Sasa Kocha Amorim ameibuka kumkingia kifua mchezaji wake, ambaye pia ni Mreno mwenzake, akisema: “Unapocheza hii timu basi uwe umejiandaa kukosolewa. Nafahamu wachezaji wa zamani walipata mafanikio makubwa sana hapa na walikuwa wakicheza kwa viwango vya juu. Wao wanaona vitu kwenye nyeusi na nyeupe. Maisha wakati mwingine si nyeusi na nyeupe — kuna rangi nyingine hivyo ni lazima ufahamu muktadha. Fernandes siku zote, anajaribu kwa ubora wake. Najivunia kuwa kocha wa mchezaji kama yeye.”
Fernandes amehusika kwenye mabao 11 katika mechi 13 za mwisho za Man United.
Amorim aliongeza: “Ni mchezaji muhimu sana kwenye timu, unaweza kuona namba zake.”
Wakati huo huo, Fernandes alifichua aligomea ofa ya kuondoka Man United dirisha la majira ya kiangazi la waka jana, wakati klabu za Saudi Arabia na Bayern Munich zilipohitaji huduma yake.
Fernandes alisema: “Nilikaa kikao na timu kwa sababu nilipata ofa. Waliniambia wanachotaka kutoka kwangu. Niliwauliza kama bado wananiona kama mimi sehemu ya maisha yao ya baadaye au la. Nilizungumza na Erik ten Hag wakati yupo. Klabu ilikuwa wazi kwangu, walionyesha naweza kuwa sehemu kubwa ya kujijenga upya. Lakini, sasa yupo chini ya kocha mpya na staili tofauti ya uchezaji. Bado nina furaha kwenye hii timu. Siku zote nina furaha kwenye hii timu. Kuichezea klabu hi ni heshima kubwa kwangu.”