Beki Arsenal avamiwa

Beki Arsenal avamiwa

London, England. BEKI wa Arsenal, Gabriel, amevamiwa na mwizi nyumbani kwake muda mchache tu baada ya kurejea nyumbani akitokea kwenye matanuzi pamoja na marafiki zake.

Gabriel alipambana na mwizi huyo aliyejaribu kuiba gari lake la aina ya Mercedes, yenye thamani ya Pauni 45,000, ndani ya maegesho yake.

Kwa mujibu wa gazeti la Sportmail, beki huyo anayekipiga Arsenal alifuatiliwa kwa makini na mwizi huyo mwenye asili ya Somalia, akiwa na marafiki zake wakati wanarudi nyumbani wakitokea kwenye matanuzi.

Mwizi huyo aliyefahamika kwa jina la

Abderaham Muse, alijaribu kumshambulia kwa rungu usoni beki huyo wa Kimataifa Brazil, hata hivyo alishindwa kutimiza azma yake ovu na kukimbia.

Kwa mujibu wa taarifa, mwizi huyo alibainika kutokana na DNA iliyopatikana katika kofia yake aliyoiangusha wakati wa purukushani kabla ya kukimbia.

Mwizi huyo hakuwa peke yake alikuwa na wenzake ambao walijificha sura huku wakiwa wameshika rungu kwa ajili ya kumshambulia nyota huyo wa Arsenal.

Gabriel aliyejiunga na Arsenal kwa kitita cha Pauni milioni 27milioni akitokea Lille mwaka jana, alijitahidi kupambana na wezi hao ambao walijaribu kuiba vitu vyake vya thamani ikiwemo gari yake aina ya Mercedes.

Taarifa njema ni kwamba hakuna maumivu yoyote aliyopata nyota huyo baada ya kushambuliwa na wezi hao kwa kutumia rungu.

Gabriel amecheza mechi 33 Arsenal tangu alipojiunga na wababe hao wa London katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka jana. Tukio hilo si mara ya kwanza kutokea kwa nyota wa Arsenal, lilimtokea pia mchezaji mwenzake wa zamani Mesut Ozil ambaye alisaidiwa na beki Sead Kolasinac, ambaye alipambana na wezi wawili mwaka 2019.