ZOO KUSHIKANA MASHATI NA FIFA

KLABU ya Zoo Kericho imeamua kama mbaya, mbaya.  Klabu hiyo sasa imetoa taarifa ikisema kuwa itakata rufaa dhidi ya FIFA baada ya chombo hicho kuichuja kwenye ligi kuu na kuiteremshwa hadi ligi ya divisheni ya kwanza (Division One League)
FIFA ilifikia uamuzi huo baada ya kuipata Zoo Kericho na makosa ya kuhusika na upangaji mechi. Hatua hiyo iliilazimu FKF kupanga pangua ratiba yake ya ligi kuu inayaorejea msimu ujao ili kuratibu upya mechi bila ya Zoo.
Sasa Zoo kupitia mwenyekiti wake Ken Ochieng imethibitisha kwamba itakataa rufaa dhidi ya uamuzi huo wa FIFA  kuwachuja kwenye ligi kuu.
Kwenye rufaa yake ambayo Zoo inapania kuwasilisha mbele ya kamati ya FIFA ya rufaa, klabu hiyo itaomba uamuzi huo usitekelezwe hadi pale kesi yao itakaposikizwa na kuamuliwa. Kwa wakati huo, itaomba Zoo iruhusiwe kuendelea kushiriki mechi zake za ligi kuu za msimu huu.
“Tayari tumeshaandaa  kesi yetu ya rufaa tutakayoiwakilisha mbele ya kamati ya FIFA inayodili na rufaa chini ya kifungu 56 cha nidhamu kwenye katiba ya FIFA. Tuna uhakika tutashinda kwenye rufaa yetu hii,” kipande cha taarifa hiyo iliyosainiwa na Ochieng ilieleza.
Kulingana na Zoo, wanataka FIFA iwape ushahidi walio nao, walioutumia kufikia uamuzi huo wa kuwatimua kutoka kwenye ligi kuu.
Mechi mbili zilizowaingiza kwenye ngori hiyo ni ile dhidi ya Sofdapaka iliyochezwa Januari 27, 2019 na Wazito FC iliyopigwa Machi 1, 2020. Mechi zote hizo zilichezewa katika uwanja wa Kenyatta Stadium.
Zoo inasema kitengo cha uadilifu cha FIFA kilichunguza madai hayo yalipozuka kutokana na mechi hizo na kufikia uamuzi kwamba hakukuwepo na kisa chochote cha upangaji mechi. Sasa klab u iashangaa uamuzi wa kuwashusha daraja uliafikiwa vipi.
Hadi uamuzi huo unafikiwa Zoo walikuwa wakikamata nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi kuu kwa alama nane baada ya mechi 14. Zoo wamekuwa kwenye ligi kuu kwa miaka mitano sasa toka walipopanda daraja.
Ochieng pia kaikashifu FKF kwa kuchukua uamuzi wa haraka na kuwachuja kwenye ligi kuu wakati FIFA imeipa Zoo Kericho siku 30 kukataa rufaa.
“Barua tuliyopokea kutoka kwa FIFA imetupa siku 30 kukataa rufaa dhidi ya uamuzi huo. Hivyo sielewi ni kwa nini FKF walikurupuka kutushusha daraja. Hili tutalikemea.”
Ikiwa rufaa yao itatupwa nje na FIFA, Zoo imedokeza kuwa itawasilisha kesi hiyo mbele ya mahakama ya kitaifa CAS (Court of Arbitration For Sports).