Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanyonyi ashinda tuzo ya dunia, autamani ubingwa wa Ultimate Championships

WANYONYI Pict

Muktasari:

  • World Athletics Ultimate Championship, yanayojulikana pia kama Ultimate Championship, ni mashindano mapya ya kimataifa ya riadha yatakayofanyika kila baada ya miaka miwili kuanzia mwaka 2026, yakihusisha wanariadha bora pekee duniani.

BINGWA wa Olimpiki na dunia katika mbio za mita 800, Emmanuel Wanyonyi kutoka Kenya, amesema analenga kuvunja rekodi yake binafsi na kuongeza taji la kwanza la mashindano mapya ya World Athletics Ultimate Championship.

World Athletics Ultimate Championship, yanayojulikana pia kama Ultimate Championship, ni mashindano mapya ya kimataifa ya riadha yatakayofanyika kila baada ya miaka miwili kuanzia mwaka 2026, yakihusisha wanariadha bora pekee duniani.

Akizungumza juzi Jumapili Novemba 30, 2025 baada ya kutangazwa kuwa Mwanariadha wa Mwaka wa Mbio za Uwanjani 2025 na Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletics) huko Monaco nchini Ufaransa, Wanyonyi, mwenye umri wa miaka 21, amesema kutwaa tuzo hiyo miaka miwili tu baada ya kuitwa Mwanariadha Chipukizi Bora wa Kiume 2023, kumempa motisha ya kutafuta mafanikio zaidi.

Alipoulizwa ikiwa kupunguza muda wake binafsi ni miongoni mwa malengo yake ya mwaka ujao baada ya kuongeza taji la dunia Septemba kwenye medali yake ya dhahabu ya Olimpiki ya Paris 2024, Wanyonyi amejibu: “Kwa nini isiwe hivyo.”

Amesema hawezi kuzungumzia sana mashindano ya Ultimate Championships kwa kuwa ni mapya, lakini ana mipango maalumu.

WANYO 01

“Natamani kufanya jambo la kipekee kwenye mashindano hayo mwakani. Inabaki kuwa siri, ila itahitaji maandalizi mazuri,” amesema.

Kocha wake, Claudio Berardelli, amesema Wanyonyi bado ana mengi ya kufanikisha katika maisha yake ya riadha.

“Hatujafikia upeo kabisa… Bado ni kijana wa miaka 21 tu na anaanza,” amesema Berardelli.

Wanyonyi aliibuka mshindi wa tuzo hiyo mbele ya Mmarekani Noah Lyles, aliyedumisha taji lake la dunia la mita 200, pamoja na kupata shaba kwenye mita 100 katika Riadha za Dunia.

Mwaka 2024, Wanyonyi aliboresha rekodi yake binafsi kwa sekunde 0.08 hadi dakika 1:41.11 alipotwaa taji la Diamond League mjini Lausanne, Uswisi. Muda huo ulimuweka sawa na Mdenmark Wilson Kipketer katika nafasi ya pili kwenye rekodi za muda wote, nyuma ya David Rudisha mwenye rekodi ya dunia ya 1:40.91 aliyoivunja kwenye Olimpiki za London 2012.

“Nawashukuru mashabiki wangu waliopiga kura duniani kote. Nimefurahi sana na nina msisimko,” amesema Wanyonyi, akitambua kuwa mbio za raundi mbili zimekuwa ngumu na zenye ushindani mkubwa. Anakuwa Mkenya wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu mfumo mpya ulipoanzishwa mwaka 2023, baada ya pia kushinda Mwanariadha Chipukizi Bora wa Kiume 2023.

Mwaka huu 2025, Wanyonyi alitoka kupoteza kwenye Diamond League ya Rabat na kisha kushinda Oslo kwa 1:42.78 Juni 12, Stockholm kwa 1:41.95 Juni 15, kabla ya kuweka rekodi ya mashindano ya 1:41.44 Julai 11 mjini Monaco alikojaribu kuivunja rekodi ya dunia.

Mshindi wa medali ya shaba ya dunia kwenye mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Edmund Serem, alishinda tuzo ya Mwanariadha Chipukizi Bora wa Kiume 2025.

Mondo Duplantis, aliyeboresha rekodi yake ya dunia mara tano mwaka huu ya mwisho ikiwa 6.30m, alipotetea taji lake Tokyo, alitangazwa Mwanariadha Bora wa Dunia 2025. Awali alikuwa ametajwa Mwanariadha Bora wa Uwanja wa Kiume.

Bingwa wa dunia wa mita 400 na mbio za kupokezana vijiti (4x400m), Sydney McLaughlin-Levrone kutoka Marekani, alishinda tuzo ya Mwanariadha Bora wa Dunia wa Kike.