WANYAMA, KAHATA, ORIGI NDO BASI TENA HARAMBEE?

Muktasari:
HUENDA ukawa ndio mwisho wa kina Victor Wanyama, Arnold Origi, Francis Kahata kuichezea Harambee Stars baada ya kocha Jacob Ghost Mulee kudokeza kaanza kukisuka kikosi kipya kabisa.
HUENDA ukawa ndio mwisho wa kina Victor Wanyama, Arnold Origi, Francis Kahata kuichezea Harambee Stars baada ya kocha Jacob Ghost Mulee kudokeza kaanza kukisuka kikosi kipya kabisa.
Kuelekea mechi dhidi ya Misri juzi Alhamisi na ya Togo Jumatatu wiki ijayo, kocha Mulee aliwajumulisha wachezaji 10 pekee wanaosakata soka lao nje ya nchi katika kikosi chake cha jumla ya wachezaji 28.
Mulee aliwaacha nje kina Wanyama, kiungo Francis Kahata, wing’a Ayub Timbe, kipa Kenya One Arnold Origi, Johanna Omollo, Eric Johanna, Patrick Matasi na Brian Mandela wakiwa ni baadhi tu ya wachezaji wazoefu waliodumu Stars kwa zaidi ya miaka 10.
Nafasi zao zilichukuliwa na sura mpya za wachezaji chipukizi wengi wao wakiwa ni wanaosakata soka lao kwenye ligi kuu ya FKF-PL.
Kwenye line-up yake dhidi ya Misri, walianza wachezaji watano pekee wanaocheza soka lao la kulipwa nje ya nchi. Kipa Ian Otieno (Zesco United), kiungo mkabaji Antony Teddy Akumu (Kaizer Chiefs), Joash Onyango (Simba SC), Masoud Juma (JS Kabylie) na Michael Olunga (Al Dhulail). Benchi ilijaa wachezaji wa ndani isipokuwa Cliff Nyakeya anayeichezea Masr FC ya Misri.
Kulingana na Mulee ambaye sasa kaanza kuelekeza nguvu zake kwenye mechi za kufuzu kushiriki kombe la dunia 2022.
“Siangali tu mechi za AFCON Misri na Togo. Tunachokifanya ni kukisuka kikosi cha siku za usoni na acha nisema kuwa siamini kwamba kila mchezaji anayesakata soka nje ya nje ni bora kuliko wanaocheza ndani. Wachezaji niliowateua nilifanya hivyo kwa kuzingatia uwezo wao wa kucheza katika kiwango cha juu. Haikua suala la kuwachuja wengine na kujaza nafasi hizo na wengine. Taratibu tumeanza kusuka kikosi kipya kabisa cha siku za usoni. Tunawaza pia mechi za kufuzu kombe la dunia.” Mulee kadokeza.
Mulee kasisistiza kuwa hataki kuingia kwenye mjadala wa kuzungumzia wachezaji alioacha nje na alioita kikosini akishikilia kwamba ana malengo ya kufanikisha kwenye mkataba wake kama kocha wa Stars.
“Sipendi kuwazungumzia wachezaji ambao hatupo nao kambini. Kuna sababu nyingi za kuwaita walioitwa ukiachia mbali fomu yao pia tulitathmini matokeo ya mechi zetu zilizopita kabla ya kufikia hapa tulipo.” Mulee kaongeza.
Jumatatu wiki ijayo Mulee atawaongoza vijana wake kwenye mechi ya mwisho ya kundi G kufuzu AFCON 2022 dhidi ya Togo.
Baada ya hapo ataanza maadalizi ya kushiriki mechi za kufuzu kombe la dunia 2022. Kwenye dimba hilo la kufuzu kombe la dunia, Kenya imepangwa kwenye kundi E pamoja Mali, Rwanda na Uganda.
Kombe la dunia 2022 litaandaliwa kuanzia Novemba ikiwa ni baada ya kufanyika kwa AFCON 2022 itakayoandaliwa kuanzia Janauri.