Wameshinda ila mdosi Ingwe amepaniki

LICHA ya kuanza msimu mpya wa FKFPL 2022/23 kwa ushindi mtamu wa mabao 2-0 dhidi ya wanajeshi Ulinzi Stars, mwenyekiti wa AFC Leopards, Dan Shikanda, bado hana imani na kikosi chake.

Kwa mtazamo wake, Shikanda anahisi kikosi chao bado ni dhaifu mno kutoa ushindani wa maana msimu huu.

“Kikosi chetu kina mapungufu sana na kusema kweli kinahitaji maboresho. Benchi la ukufunzi limenifahamisha kuwa tunahitaji kufanya usajili na ndio sababu nina hofu kidogo licha yetu kuanza vizuri,” alisema Shikanda ambapo Jumamosi iliyopita, AFC Leopards ilikosa huduma ya wachezaji wake 10 wanaounda kikosi cha kwanza waliyoshindwa kusajiliwa kutokana na marufuku ya FIFA dhidi ya Ingwe.

Wachezaji hao ni Cliff Nyakeya, Josphat Lopaga, Victor Omune, Musa Oundo, Emmanuel Lwanga, Ronald Sichenje, Loren James, Victor Otieno, Aboubakar Musha na Nesta Olum.