Ushindi mnono wampagawisha Kimani

KOCHA wa Bandari FC, Anthony ‘Modo’ Kimani, alisema anatamani sana kuona yale aliyashuhudia mastraika wake wakiyafanya walipocheza na Ulinzi Stars FC yakiendelea katika mechi zingine.

Akiongea na MWANASPOTI, Kimani alisema alifurahia wachezaji wake walivyotumia vizuri nafasi zao za kufunga mabao matano dhidi ya wanajeshi hao.

“Tumekuwa na tatizo la kupoteza nafasi nyingi katika mechi zetu lakini wanasoka wangu walitumia vizuri nafasi walizozipata tukaweza kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Ulinzi,” alisema.

Kimani alikumbusha jinsi vijana wake walivyopata kona 12 walipocheza na Mwatate United lakini hakuna hata moja iliyozalisha matunda na akawasifu kwa kufunga mabao matatu dhidi ya Ulinzi kupitia kona walizopata.

Aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa nguvu na ari dakika zote 90 za jambo lililochangia kupatikana ushindi huo mkubwa.

Katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Mbaraki Sports Club katikati ya wiki hii, mabao ya Bandari yalifungwa na Rogers Aloro na Umara Kasumba ambao wote waliweka kambani mabao mawili kila mmoja na lingine likapachikwa na Douglas Mokaya.

Mkufunzi huyo wa Bandari alisema ana matumani vijana wake wataendelea kutumia nafasi zao vizuri kwenye mechi zao zijazo, wakianzia dhidi ya Kakamega Homeboys watakayocheza ugenini kesho Jumapili