Ukiachwa utaambia nini watu!

KLABU zinazofukuzia ubingwa Ligi Kuu Kenya msimu huu ziko bampa to bampa ambapo ukiachwa unajiwekewa mazingira magumu kuwa miongoni mwa farasi zinazofukuzia ubingwa.

Gepu la pointi moja ndilo linalowatenganisha Nzoia Sugar waliyoachia usukani wa FKFPL kwa Gor Mahia huku KCB ikizidiwa kwa pointi tatu na vinara wapya K’Ogalo wakati huwezi kuwatoa kwenye hesabu Kenya Police FC, AFC Leopards na Tusker FC.

Mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia, watakuwa wageni wa Ulinzi Stars katika mechi kali itakayopigwa leo Jumamosi Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Chini ya ukufunzi wa Jonathan McKinstry, Gor Mahia ambayo ipo kileleni mwa msimamo FKFPL na pointi zake 33, wameshinda mechi nne kati ya tano za mwisho wakiambulia sare moja tu.

Macho yatakuwa kwa straika Benson Omala ambaye Jumanne ya wiki hii alifunga hat-trick yake ya pili msimu huu na kuisaidia K’Ogalo kuisambaratisha Wazito FC mabao 4-0.

Kocha McKinstry alinukuliwa baada ya mchezo huo akisema fomu nzuri ya Omala inatokana na kugusa mpira mara chache pamoja na pasi nzuri anazopokea kutoka kwa wachezaji wenzake.

“Uhalisia wa straika mnoma ni kuwa na miguso michache na unapopata miguso hiyo ni pale upo ndani ya boxi au upo uso kwa uso na kipa,” alisema McKinstry alipokuwa anazungumzia fomu balaa ya Omala ambaye hadi sasa anaongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu akiwa ashatupia kambani mabao 15.

Ulinzi Stars inayofundishwa na aliyewahi kuwa straika wa Harambee Stars, Bernard Mwalala, inaikabili Gor Mahia ikitoka kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Bidco huku wakiwa wameshinda mchezo moja kati ya mitano za mwisho.

Hata hivyo, akiongea na mtandao wa klabu yake, nahodha msaidizi wa Ulinzi Stars, Brian Birgen, alisema wanaimani kuondoka na pointi tatu japo alikiri mechi hiyo itakua ngumu.

“Tunajua itakua gemu ngumu na tutajaribu kila liwezekanalo kuonyesha ubora wetu na tayari kocha ametuweka sawa hivyo wachezaji wote wapo tayari,” alisema Birgen.  

Nzoia Sugar nao watakua nyumbani kwenye Uwanja wa Sudi, Kanduyi kaunti ya Bungoma kuwakaribisha Posta Rangers.

Kocha Salim Babu amewasisitizia vijana wake kuelekeza mawazo yao kushinda mechi zao pasipo kuangalia matokeo ya wapinzani wao kwani kufanya hivyo itawaondolea presha.

KCB yake Zedekiah ‘Zico’ Otieno ambayo ipo nafasi ya tatu na pointi 30 inasaka ushindi wa tatu mfululizo itakapokuwa wageni wa vibonde Vihiga Bullets kesho Jumapili katika Uwanja wa Bukhungu kaunti ya Kakamega.

Mabingwa watetezi Tusker FC ambao wamepotea mwelekeo baada ya kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Gor Mahia mchezo wao wa mwisho, wamepania kuzinduka kwa Mathare United leo Jumamosi Uwanja wa Ruaraka, Nairobi, lakini wanafahamufika wataikabili Mathare iliyoshinda mechi mbili za mwisho na kujitoa mkiani mwa msimamo FKFPL.

AFC Leopards, wakali wa kukusanya mashabiki na wakiwa freshi baada ya kuvuna ushindi mkubwa wa mabao 6-0 dhidi ya FC Talanta, watashuka katika uga wa Nyayo jijini Nairobi kesho Jumapili kuendeleza dozi zingine dhidi ya Kariobangi Sharks waliyochezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mathare United.  


RATIBA KAMILI FKFPL

LEO JUMAMOSI

Wazito v Bandari

Bidco v Sofapaka

Homeboyz v City Stars

Nzoia Sugar v Rangers

Police FC v Talanta

Tusker v Mathare

Ulinzi v Gor Mahia


KESHO JUMAPILI

Leopards v Sharks

Vihiga v KCB