Tusker, Coastal zapeleka furaha Moshi

WADAU wa Soka mkoani Kilimanjaro watapata bahati ya kushuhudia mchezo wa kirafiki wa Kimataifa baina ya timu za Tusker FC kutoka Kenya na Caostal Union ambayo itapigwa katika Uwanja wa Ushirika uliopo Manispaa ya Moshi.

Mchezo huo kwa timu zote itakuwa ni maalum kwa ajili ya kuendelea kuimarisha vikosi vyao kabla ya kuanza msimu wa 2023/24 kwa Ligi zao, Ligi Kuu Bara ambayo itaanza Agosti 15, Coastal wakitoka nje mechi tatu kucheza ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar na Simba.

Mpaka sasa timu hiyo inayonolewa na kocha Mwinyi  Zahera imecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Mombasa Kenya ambapo ilipoteza kwa goli 1-0,na kuichapa goli 1-0 Singida Fountain Gate.

Tusker FC ambayo imeweka kambi ya maandalizi jijini Arusha ikijiandaa na michuano ya Ligi Kuu Kenya FKFPL huku ikianzia ugenini Agosti 26 dhidi ya Bandari FC ya Mombasa,kabla ya kuja Tanzania ilicheza mchezo mmoja wa kirafiki na timu ya Plantech ya huko kwao na kushinda goli 6-0.

Afisa habari wa timu ya Tusker FC,Timothy Olobulu amesema mchezo huo kwao ni muhimu kwani itamsaidia kocha Robert Matano kuweza kuona ni namna gani vijana wake wanafanyia kazi maelekezo ambayo anawapatia.

Ameongeza kuwa pia itasaidia timu kupata muunganiko ili Ligi ikianza basi iweze kufikia malengo ambayo imejiwekea kwa maana ya kufanya vizuri na kutwaa ubingwa.

Amesema baada ya mchezo wa kesho timu yao  itacheza  tena mechi  mbili za kirafiki dhidi ya Vital’O kutoka Burundi siku ya Ijumaa na Mbuni FC ya Arusha inayoshiriki Championship,mechi hizo zitapigwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Katibu wa Chama Cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA),Harold Kifunda amethibitisha uwepo wa mechi kati ya Coastal Union na Tusker FC na kuweka wazi  kiingilio kitakuwa ni buku tatu pekee Sh3000.

Amesema mchezo huo utatoa fursa kwa wakazi wa Moshi kushuudia ladha ya burudani ya Soka la Kimataifa ambapo pia anaamini itaijenga Coastal Union ambao ndio timu pekee kutoka Kanda ya Kaskazini inayoshiriki Ligi Kuu Bara baada ya Polisi Tanzania FC kushuka daraja msimu uliopita.