Taji KWPL lawanukia Gaspo Women

NAIROBI. HUKU zikiwa zimesalia mechi nane pekee Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) kukamilika, Gaspo Women kwasasa wako kileleni mwa jedwali na alama zao 31 wakifuatiwa na Vihiga Queens.

Hivi karibuni Gaspo ambayo safu yake ya ushambuliaji inaongoza kupachika mabao mengi huku safu ya ulinzi ikiruhusu mabao machache, ilimtambulisha Jacob ‘Ghost’ Mulee kuwa kocha wao mpya.

“Nilipenda jinsi wanavyocheza, na niko hapa kusaidia kuinua kiwango cha timu kutokana na uzoefu wangu,” alisema Mulee.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alisema kuna ushindani mkubwa kaika ligi ya wanawake akiitaja Vihiga Queens ambao wamekuwa mabingwa kwa muda mrefu, na upinzani unaotoka kwa timu nyingine nzuri kama vile Zetech Sparks na Ulinzi Starlets.

Kibarua cha kwanza kwa Mulee ni kesho Jumapili dhidi ya Zetech Sparks mechi itakayopigwa uwanja wa GEMS Cambridge Rongai kaunti ya Kajiado.

Kiungo wa kati wa Gaspo Women, Lydia Akoth, amefunga jumla ya mabao saba msimu huu na alirejea maoni ya kocha huyo ya kushinda ligi.

“Tutachukua pointi tatu katika dimba la GEMS, msimu huu lazima tuchukue kombe na ili kufanya hivyo lazima tuchukue ushindi katika mechi nane zijazo,” alisema Lydia.

Wikendi hii ya Pasaka, Ulinzi Starlets wanasafiri hadi Kisumu kucheza na Kisumu All Starlets ikiwa ndiyo mechi ya pekee leo Jumamosi na kesho Vihiga Queens watamenyana na Trans Nzoia Falcons uwanjani Mumias Sports Complex, Kangemi Ladies ikivaana na Kayole Starlets ugani Camp Toyoyo, Nakuru City Queens uso kwa uso na Thika Queens nayo Bunyore Starlets ikigaragazana na Wadadia.