Chozi la Diamond, Kiba kwa Raila Odinga
Muktasari:
- Hayati Odinga alikuwa karibu na wanamichezo na wasanii ambao baadhi aliwahi kuwaalika kutumbuiza katika kampeni zake, jambo ambalo limeonekana kuwagusa zaidi.
KUNA siri kubwa ya wanamichezo na wasanii nchini kuumizwa na kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliyefariki dunia nchini India, Agosti 15, 2025.
Hayati Odinga alikuwa karibu na wanamichezo na wasanii ambao baadhi aliwahi kuwaalika kutumbuiza katika kampeni zake, jambo ambalo limeonekana kuwagusa zaidi.
Ukiacha hilo nchini Kenya alifanya mengi katika michezo na burudani pia alikuwa mlezi wa klabu ya Gor Mahia na mtu wa kujitoa zaidi kwa wananchi wa hali ya chini ambao katika msiba huo wanaonekana kuguswa zaidi.
Mchezaji wa Gor Mahia aliyejitambulisha kwa jina la Joshua Onyango anasema: "Ametuachia huzuni kubwa itakayotuchukua muda mrefu kumsahau, alikuwa baba mzuri. Kuna wakati alikuwa anatupigia simu akitaka kuja uwanjani na kutuambia tusimwangushe, alikuwa na upendo mkubwa ikitokea tumevunjika moyo alituambiwa tusikate tamaa kwani maisha yana kupanda na kushuka."
Bahati, nyota wa muziki wa kizazi kipya wa Kenya, ameandika wimbo wa maombolezo ya msiba huo unaoenda kwa jina la Bye Bye ambao ndani yake unazungumzia upendo wa Odinga kwa jamii.
Mwaka 2015 Azam FC ilipokuwa imechukua ubingwa wa Kombe la Kagame, Odinga ndiye aliyemkabidhi Kombe aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco.
Katika tukio hilo Odinga alifuatana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, na wachezaji walioonekana katika picha hiyo ni Didier Kavumbagu, Himid Mao, Aishi Manula, Gadiel Michael.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wasanii ambao wameguswa na msiba huo kutokea Tanzania na kiongozi mkuu wa mpinzani kwa chama tawala nchini Kenya cha United Democratic Alliance kinachoongozwa na Rais William Ruto.
MWANA FA
Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' msanii wa Hip Hop na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), alionyesha kusikitishwa na msiba wa Ruto kupitia maandiko katika ukursa wa Instagram.
"Tangulia Kiongozi, njia yetu ni moja, umeifanya kazi iliyokuleta duniani kwa uaminifu mkubwa, ukapumzike kwa amani. RIP Baba.'
ALIKIBA
Msanii wa Bongo Fleva aliyeoa Kenya na kuzaa watoto wawili na mkewe Amina, ameandika ujumbe kwa lugha ya Kiingereza kuhusiana na kusikitishwa na msiba wa Odinga.
Kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, sehemu ya ujumbe huo unasomeka hivi: "Nimesikitishwa sana na kifo cha Mhe. Raila Amolo Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya. Kwa niaba yangu na wale wote wanaokuheshimu, natoa salamu zangu za rambirambi kwako na kwa familia yako katika kipindi hiki cha majonzi.
"Uthabiti wako na moyo wako usioyumbayumba umewatia moyo watu wengi kote nchini kwa muda mrefu, na tunaamini kwamba nguvu hiyo hiyo itatuongoza katika kipindi hiki kigumu."
DIAMOND
Mwaka 2022 katika kampeni za mwisho za Odinga za kuwania Urais kupitia chama cha Azimio la Umoja Coalition Kasarani, alimwalika msanii wa Bongo Fleva kutoka Tanzania, Diamond Platnumz kutumbuiza kwenye Uwanja wa Nairobi nchini Kenya.
Diamond aliimba wimbo wa Waah ft Koffi Olomide na kisha akamwambia maneno: "Baba nataka nikwambie, vijana wanakuamini sana na wewe ndiye Rais wetu unayefuata."
Katika mtandao wa kijamii wa Instagram supastaa huyo ameandika: "Mwenyezi Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi."
ERIC OMONDI
Mchekeshaji wa Kenya, Eric Omondi katika mtandao wa kijamii wa Instagram aliweka video ambayo Hayati Ondinga alikwenda kumpa pole baada ya kufiwa na kaka yake Fredy mwaka jana.
Video ya pili aliyoweka Omondi katika mtandao huo inamuonyesha akiwa anamfariji mke wa Hayati Ondinga na kuandika: "Nimemtembelea mama yangu asubuhi, tunahitaji kuiombea familia na apumzike kwa amani baba yangu."
OTILE BROWN
Msanii Otile Brown wa Kenya aliyewahi kufanya kolabo na wasanii mbalimbali wa Tanzania kama wimbo One Call ft Ruby na Woman ft Harmonize, katika mtandao wa kijamii wa Instagram ameweka picha ya Hayati Odinga na kuandika: "Asante sana baba, lala salama shujaa."
HARMONIZE
Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize anasema: "Watu wangu wa Kenya poleni sana kwa kumpoteza baba, niko pamoja nanyi katika kipindi kigumu, tunaomboleza kwa pamoja katika hizo siku saba zilizotangazwa na Rais William Ruto."
Wachekeshaji wa Tanzania, Steve Mweusi na Ndaro, hawakuwa nyuma katika kutoa salamu zao za pole kwa watu wa Kenya kwa kuondokewa na Hayati Odinga.
"Ukiondoa Watanzania kutusapoti kazi zetu za sanaa, wanaofuatia ni Wakenya, tumeumizwa na msiba huo, tunawaombea kwa Mungu awavushe salama katika kipindi kigumu mnachokipitia," anasema Steve.
"Inaumiza sana lakini hatuna budi kumuombea kwa Mungu baba yetu Odinga alale salama na kazi alizozifanya zitakumbukwa daima, poleni ndugu zetu Wakenya tupo pamoja katika kipindi kigumu mnachokipitia," anasema Ndaro.