Harambee Stars yafukuzia bao la 100 ikiikabili Ivory Coast leo
Muktasari:
- Kwa Kenya, licha ya kwamba haina nafasi yoyote ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, lakini inahitaji kufunga bao moja tu kuweka rekodi ya kufikisha mabao 100 katika harakati zake za kufuzu Kombe la Dunia kwenye historia ya nchi hiyo.
LEO Oktoba 14, 2025, itakuwa siku ya kukumbukwa zaidi na mataifa mawili ya Ivory Coast na Kenya, hiyo ni baada ya kumalizika kwa dakika tisini za mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026. Kumbukumbu inayosubiriwa na kila upande ni ile ya kufurahisha zaidi, lakini kinyume chake inaweza kuumiza.
Kwa Kenya, licha ya kwamba haina nafasi yoyote ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, lakini inahitaji kufunga bao moja tu kuweka rekodi ya kufikisha mabao 100 katika harakati zake za kufuzu Kombe la Dunia kwenye historia ya nchi hiyo.
Katika historia yao ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Kenya imefunga mabao 99, na inaweza kufikisha bao la 100 leo jijini Abidjan, ikiwa ni baada ya kucheza mechi 83 za kufuzu.
Bao la kwanza la Kenya katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia lilifungwa miaka 53 iliyopita na Daniel Anyazwa dhidi ya Sudan mnamo Julai 6, 1972 katika ushindi wa 2-0.
Mshambuliaji Ryan Ogam, mwenye umri wa miaka 21, ndiye aliyefunga bao la 99 dhidi ya Burundi na sasa ana jumla ya mabao sita katika mechi 6 za timu za taifa, huenda yeye ndiye atakayeingia kwenye historia kwa kufunga bao la 100.
Akizungumza akiwa Abidjan, Ogam amesema kuna furaha na shinikizo kubwa kuvaa jezi inayowakilisha mamilioni ya Wakenya.
“Ninataka kuendelea kujituma na kuendeleza rekodi ya kufunga kila mechi, kwa klabu na taifa. Nataka pia kuhamasisha wachezaji chipukizi waamini kuwa inawezekana,” amesema Ogam.
Hata hivyo, Harambee Stars ina kazi ngumu dhidi ya Ivory Coast ambayo haijaruhusu bao hata moja katika mechi zote za kufuzu Kundi F ikiwa kileleni kutokana na kucheza mechi tisa, imeshinda saba na sare mbili.
“Tunajua ubora wa kikosi chao, hawajapoteza mechi yoyote katika kampeni hii. Lakini tunaamini katika uwezo wetu,” amesema kocha msaidizi wa kikosi cha Kenya, Vasili Manousakis.
Ivory Coast inayoshika nafasi ya 44 katika viwango vya soka duniani, inajivunia nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa katika klabu maarufu Ulaya. Kenya kwa sasa iko nafasi ya 111 duniani.
Ivory Coast inaweza kujiunga na mataifa machache yaliowahi kufuzu kwa Kombe la Dunia bila kuruhusu bao ambayo ni Italia (1934 na 1974), Uturuki (1950), Yugoslavia (1954), Uruguay (1970), Chile (1982) na England (1990).
Cha kufurahisha kwa Kenya ni kuwa, Harambee Stars ndiyo timu pekee katika Kundi F ambayo Ivory Coast haijapata ushindi mbele yao. Mechi ya mkondo wa kwanza ilimalizika kwa matokeo ya 0-0, ikifanyika nchini Malawi, Kenya ikiwa mwenyeji.
Kenya ina matumaini kwamba haijapoteza mechi yoyote iliyopigwa jijini Abidjan katika mbio hizi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwani ilitoka sare ya 3-3 dhidi ya The Gambia na kuicharaza Seychelles 5-0, zote zilichezwa Abidjan.
Ivory Coast maarufu kama Tembo, itakabiliana na Harambee Stars katika mechi muhimu ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026, itakayopigwa leo Jumanne kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara, Abidjan kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Ushindi kwa wenyeji utaihakikishia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026 nchini Canada, Mexico na Marekani.
Hata hivyo, sare au kichapo dhidi ya Kenya kutamaanisha kuwa Ivory Coast itahitaji Gabon pia ishindwe kupata ushindi nyumbani dhidi ya Burundi ili kufuzu moja kwa moja.
Kwa sasa, Ivory Coast inaongoza Kundi F ikiwa na pointi 23, ikifuatwa na Gabon yenye pointi 22. Kenya ni wa tatu na pointi 12, kisha The Gambia na Burundi zenye pointi 10 kila mmoja. Seychelles inasalia mkiani bila pointi.
“Soka huchezwa uwanjani, si kwa karatasi. Ivory Coast wasitarajie upendeleo kutoka kwetu. Tumekuja kushinda, na iwapo wanataka kufuzu, basi wajitume vilivyo,” amesema Kocha Mkuu wa Kenya, Benni McCarthy.
“Tunalenga kumaliza kwa heshima na kukuza fikra ya ushindi. Hatutacheza kwa kujilinda nyuma. Tumeshinda mechi mbili zilizopita na hatukuruhusu bao, hiyo ni kasi tunayopaswa kuendeleza,” akaongeza msaidizi wake, Vasilis Manousakis.
Kenya iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Seychelles mwezi uliopita jijini Nairobi, kabla ya kuichapa Burundi 1-0 jijini Bujumbura wiki iliyopita.