Nahodha Gor adai Top 4 ni kubaya

KAPTENI wa Gor Mahia, Philemon Otieno, kasisitiza ni mapema mno kuwapigia upatu kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu licha ya kushika usukani.

Gor walishika usukani wa FKFPL baada ya sare ya bao 1-1 Jumamosi iliyopita dhidi ya Ulinzi Stars.

Ingawaje Gor wangali na mechi moja kibindoni ambayo kwamba wakishinda watafungua mwanya kwa alama nne kati yao na nambari mbili KCB, Otieno haioni hiyo kama fursa kubwa sana kwao.

K’Ogalo wana alama 34 baada ya mechi 15 wakifuatiwa na KCB ambao ghafla wameamsha tena mzuka wakiwa wamekusanya alama 33 kutokana na mechi 16.

Nzoia Sugar ambao kwa zaidi ya miezi miwili waligandia kileleni wameteremka hadi nafasi ya tatu wakiwa na alama 32 baada ya mechi 16 vile vile huku Kenya Police wakiwa na alama 28 kutokana na mechi 15 katika nafasi ya nne.

“Kama timu tunachojua ni kwamba timu yeyote kwenye Top 4 inayo nafasi ya kutwa ubingwa na ndio sababu hilo wazo la kuwa tuna nafasi kubwa, bado hatukubaliani nalo. Tazama msimamo wa jedwali baada ya raundi ya 16, timu zote zilizoko kwenye Top 4 zimeachana na alama mbili, tatu au nne hivi. Hii inakuonyesha ni jinsi gani ushindani ulivyo mkali kwa hiyo hatutaki kujipa presha ya namna hiyo eti kwasababu tupo kileleni,” Otieno alisisitiza.

Nahodha huyo anashikilia kuwa mpango kazi wao kwasasa ni kuipigia hesabu mechi moja baada ya nyingine kuhakikisha wanasajili ushindi.

“Ndio mpango tulionao halafu mwisho wa msimu tutafanya hayo mahesabu lakini kwasasa, hatutaki kujizengua sababu kwenye mpira lolote laweza kutokea,” alisema Otieno.

Gor hawajashinda ubingwa wa ligi kuu kwa misimu miwili sasa na matumaini yao ni makubwa mwaka huu.