Mwamuzi Mary Njoroge kuanza kazi rasmi Kombe la Dunia

Mwamuzi wa Fifa, Mary Njoroge atakuwa mmoja wa waamuzi katika mechi ya Kundi E ya Kombe la Dunia la Wanawake 2023 kati ya Ureno na Vietnam kwenye Uwanja wa Waikato, Hamilton nchini New Zealand Alhamisi.
Hili likiwa Kombe lake la pili la Dunia analochezesha, Njoroge ndiye Mkenya pekee anayesimamia michezo hiyo. Atakuwa mwamuzi msaidizi wa pili katika mechi hiyo ambapo Mnyarwanda Salima Mukansanga atakuwa mwamuzi wa kati.
Victoire Queency wa Mauritius na Anahi Fernandez wa Uruguay watakuwa mwamuzi msaidizi wa kwanza na mwamuzi wa nne mtawalia.
Njoroge, 38, pia alikuwa mwamuzi msaidizi wa Mukasanga katika Kombe la Dunia la Ufaransa U-20 2018, Kombe la Dunia la Ufaransa 2019 na Mashindano ya Soka ya Olimpiki ya Tokyo 2020.
Mkenya huyo aliondoka nchini Julai, 7, 2023 kuelekea Australia baada ya kuagws na Naibu Kamishna Mkuu wa Australia Linda Gellard katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kaunti ya Kiambu.
Katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi, Ureno ilifungwa 1-0 na Uholanzi huku Vietnam ikilala 3-0 na mabingwa watetezi Marekani.
Marekani wanaongoza Kundi E wakiwa na pointi tatu, sawa na Uholanzi walio nafasi ya pili lakini tofauti ya mabao ya juu zaidi. Ureno na Vietnam zinafuata katika nafasi ya tatu na ya nne mtawalia bila pointi.
Fifa ilikuwa iliteua waamuzi 19 wasaidizi wa video (VAR) kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia la Wanawake huku sita kati yao wakiwa ni wanawake. Adil Zourak kutoka Morocco ndiye mwakilishi pekee wa kiume kutoka Afrika.
Jumla ya waamuzi 33, waamuzi wasaidizi 55 walichaguliwa kutoka katika vyama sita vya Fifa. Afrika ilikuwa na waamuzi wa kati wanne pekee akiwemo Mukasanga. Wengine ni; Vincentia Amedome (Togo), Bouchra Karboubi (Morocco) na Akhona Makalima (Afrika Kusini).
Waamuzi wengine wasaidizi wa Afrika ni pamoja na; Carine Atezambong Fomo (Cameroon), Diana Chikotesha (Zambia), Soukaina Hamdi (Morocco), Fatiha Jermoumi (Morocco), Fanta Kone (Mali) na Queency Victoire (Mauritius).
Ni kwa mara ya kwanza jumla ya timu 32 zinashiriki michuano hiyo kutoka 24 za awali.
Mechi ya ufunguzi ilipigwa kati ya New Zealand na Norway katika uwanja wa Eden Park huko Auckland mnamo Julai 20, 2023 ambapo wenyeji walishinda 1-0.
Fainali itafanyika tarehe 20 Agosti 2023 kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Sydney huko Sydney.