Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mserbia amrithi Ndayiragije Kenya Police

Muktasari:

  • Ndayiragije aliyeiongoza Kenya Police kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita 2024-2025, aliachana na klabu hiyo Oktoba 29, 2025 baada ya siku 333 za kuhudumu ndani ya kikosi hicho.

KENYA Police FC imemuajiri kocha mpya kutoka Serbia, Dusan Stojanovic, ikiwa ni siku chache baada ya Ettiene Ndayiragije kuachana na klabu hiyo kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Ndayiragije aliyeiongoza Kenya Police kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita 2024-2025, aliachana na klabu hiyo Oktoba 29, 2025 baada ya siku 333 za kuhudumu ndani ya kikosi hicho.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44, alitambulishwa rasmi kama kocha mpya wa Kenya Police FC katika mkutano na wanahabari uliofanyika baada ya sare tasa dhidi ya Posta Rangers kwenye Uwanja wa Police Sacco, siku ya Jumapili Novemba 2, 2025.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nyale Munga, ndiye aliyeongoza hafla hiyo, akimtambulisha Stojanovic kama mrithi wa Ndayiragije.

Katika taarifa iliyotolewa siku hiyo, Kenya Police FC ilimpongeza Ndayiragije kwa mafanikio yake, ikiwemo kuipa klabu ubingwa wa kwanza wa ligi kuu msimu uliopita.

“Etienne ana nafasi maalum katika historia ya Kenya Police FC. Uongozi wa klabu unamtakia kila la heri anapokabiliana na changamoto mpya katika taaluma yake,” imesema taarifa ya klabu.

Wakati wa kumtambulisha kocha mpya, Munga amesema: “Stojanovic ana uzoefu mkubwa. Amefanya kazi Afrika Mashariki, Kaskazini, na Kusini mwa Afrika. Tumeamua kumchukua kwa sababu tunaamini uzoefu wake utatupeleka juu zaidi.”

Matarajio ya mashabiki wa Kenya Police ni kuona Stojanovic anaiongoza timu hiyo kwa mafanikio na kudumu kwa muda mrefu tofauti na ilivyokuwa kwa Zdravko Logarusic raia wa Croatia aliyekaa kwa siku 82 pekee. Logarusic pia amewahi kuzinoa AFC Leopards na Gor Mahia zote za Kenya.

Kati ya makocha sita waliowahi kuajiriwa kwa muda kamili tangu Kenya Police FC ipande daraja Juni 2021, John Boby Ogolla, Sammy ‘Pamzo’ Omollo, Francis Baraza, Salim Babu, na Etienne Ndayiragije, rekodi zinaonyesha Logarusic ndiye amekaa kwa muda fupi zaidi. Wengine waliohudumu kwa muda mfupi wakiwa makocha wa muda ni Iddi Salim, Beldine Odemba, na David Bujego.

Stojanovic ana leseni ya ukocha ya UEFA A. Amewahi kuifundisha SC Villa ya Uganda, kabla ya hapo alihudumu kama kocha msaidizi katika klabu ya Serbia, Zeleznicar Pancevo kwa siku 68 pekee. Pia amewahi kufanya kazi kama msaidizi katika kikosi cha Rad (siku 65), OFK Zarkovo (siku 24), na Zamalek ya Misri (siku 107).

Kabla ya hapo, alipita katika klabu za Serbia kama OFK Beograd (2005–2012), FK Cukaricki (2013–2016), Crvena Zvezda (2018–2019), FK Vojvodina (2021–2022), na pia klabu ya Urusi, Krasnodar (2016–2017).

Kile kinachowapa Kenya Police FC imani zaidi ni mafanikio yake ya hivi karibuni Afrika, alipokuwa kocha wa SC Villa, akiiwezesha timu hiyo ya Uganda kushinda ubingwa wa ligi msimu uliopita baada ya miaka 20. Hata hivyo, hakumaliza mkataba wake wa miaka miwili kwani alifutwa kazi Julai 2024, mwaka mmoja tu tangu ajiunge na kikosi hicho.

Pamoja na uzoefu wake Afrika Mashariki, Stojanovic amekiri kutokuwa na uzoefu wa kutosha kuhusu soka la Kenya.

“Nitakuwa mkweli. Sina uzoefu mkubwa wa soka la Kenya zaidi ya kuona vipande vya mechi nikiwa Ulaya. Hiyo peke yake haitoshi,” amesema katika utambulisho wake.

Stojanovic ni kocha wa kumi kuiongoza Kenya Police FC tangu ipande daraja mwaka 2021, hakuna timu nyingine ya ligi kuu yenye mzunguko wa makocha wengi kama huo.

Kwa wastani, makocha hukaa siku 197 pekee kabla ya kuondoka Kenya Police FC, huku Murang’a Seal pekee ikiwa na wastani mdogo zaidi (siku 137).

Kwa kuzingatia mzunguko huo mkubwa wa makocha na takwimu kwamba muda wa wastani wa kazi kwa makocha wa kigeni Kenya ni siku 257 ukilinganishwa na siku 322 kwa wazawa, bado haijulikani kama Kenya Police FC wamepata mtu wa kutekeleza mradi wa muda mrefu wa klabu.

Hata hivyo, Stojanovic anaamini yeye ndiye mtu sahihi akisema: “Mradi na maono ya Kenya Police FC yamenivutia. Tunataka kuwa juu kabisa barani Afrika.”

Munga naye akamkaribisha kwa maneno ya matumaini akisema: “Kocha, karibu sana. Watu wa Kenya ni wakarimu sana na utapenda kufanya kazi hapa.”

Mechi yake ya kwanza itakuwa nyumbani dhidi ya Sofapaka, kesho Jumatano, Novemba 5, 2025 katika Uwanja wa Police Sacco kuanzia saa 9 alasiri.