Kiungo Harambee Stars, Ouma ajiunga na Slavia Prague ya Czech.

Muktasari:
- Ouma alisema: "Ni hisia nzuri. Najiandaa kuingia uwanjani, kujitahidi kuwa mchezaji bora, tofauti. Nitajitahidi kwa kila hatua, aminia." Aliongeza: "Uwanja ni mzuri, mkubwa. Nilikuwa tu mjini kwa muda mfupi, lakini niliona kuwa Prague ni jiji zuri. Hii ni mara yangu ya kwanza hapa, nadhani nitajisikia vizuri."
Kiungo wa Harambee Stars, Timothy Ouma, amejiunga na klabu ya Slavia Prague ya Czech kwa mkataba wa miaka minne. Mabingwa hawa mara 21 wa Ligi Kuu ya Czech walitangaza usajili wa Ouma mwenye umri wa miaka 20 kupitia mitandao yao ya kijamii Jumapili.
Ouma alisema: "Ni hisia nzuri. Najiandaa kuingia uwanjani, kujitahidi kuwa mchezaji bora, tofauti. Nitajitahidi kwa kila hatua, aminia." Aliongeza: "Uwanja ni mzuri, mkubwa. Nilikuwa tu mjini kwa muda mfupi, lakini niliona kuwa Prague ni jiji zuri. Hii ni mara yangu ya kwanza hapa, nadhani nitajisikia vizuri."
Alisema kwamba ilikuwa si rahisi kufanya uamuzi huo, lakini alikaa na wakala wake na hatimaye walikubaliana kuwa Slavia Prague itakuwa chaguo bora kwake. "Slavia ni timu kubwa yenye wawakilishi wengi. Siwezi kusubiri kujiunga na wachezaji. Tutashuhudia jinsi sehemu inayofuata ya msimu itakavyokuwa kwetu sote," aliongezea.
Klabu ya Slavia inaripotiwa kumlipa kiasi cha Sh milioni 473 kwa ajili ya kiungo huyu kutoka klabu ya IF Elfsborg ya Sweden. Mkataba wake utamalizika mwezi Juni 2029.
Inaripotiwa kwamba klabu kadhaa za Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikimwania saini ya Ouma. Kiungo huyu alijiunga na Elfsborg mwaka 2022 akitokea Nairobi City Stars ya Kenya. Alijiunga na City Stars mnamo Julai 2020 baada ya kumaliza masomo yake katika Shule ya Laiser Hill Academy. Alipata wito wake wa kwanza kwa Harambee Stars Oktoba 2021 chini ya kocha wa zamani Engin Firat.