Simulizi ya Raila Odinga alivyoihama Man United na kuisapoti Arsenal hadi kifo chake
Muktasari:
- Kifo chake kimezua simanzi kubwa na salamu nyingi za rambirambi, ikiwemo kutoka kwa wadau wa soka, ambapo Raila alijulikana kama shabiki na mdhamini mkubwa wa mchezo huo.
Raila Odinga, mwanasiasa mkongwe wa Kenya na Waziri Mkuu wa zamani, amefariki dunia Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80, baada ya kupata shambulio la moyo alipokuwa akipatiwa matibabu nchini India.
Kifo chake kimezua simanzi kubwa na salamu nyingi za rambirambi, ikiwemo kutoka kwa wadau wa soka, ambapo Raila alijulikana kama shabiki na mdhamini mkubwa wa mchezo huo.
Katika moja ya mahojiano yake kabla ya kufariki, Raila alifichua kuwa hapo zamani alikuwa shabiki wa Manchester United katika miaka ya 1970.
Hata hivyo, alikata tamaa na timu hiyo baada ya kipindi cha vurugu za mashabiki kusababisha mechi nyingi kuchezwa bila watazamaji.
“Manchester United ilicheza katika uwanja mtupu kwa mwaka mmoja, ndipo nikahama kidogo kwenda Liverpool, kisha baadaye nikajikuta Arsenal,” alisema.
Raila hakuwa tu shabiki wa Arsenal kwa maneno, aliwahi kuhudhuria mechi kadhaa katika Uwanja wa Emirates, ikiwemo pambano kati ya Arsenal na Liverpool mwaka 2022.
“Mimi ni ‘Arsène Wenger Arsenalian,’ na sisi ndio klabu pekee tuliyowahi kuwa na ‘Invincibles,’” alisema katika mahojiano ya awali.
Pia alionekana mara kadhaa akiangalia mechi za Arsenal wakati wa safari zake, ikiwemo mchezo dhidi ya West Ham alipokuwa akipokea matibabu Dubai.
Raila alikuwa na uwezo wa kutaja majina ya wachezaji, kukumbuka mechi za kihistoria na kutetea kwa bidii mtindo wa uchezaji wa timu yake pendwa.
Raila ambaye mara nyingi aliitwa kwa majina ya upendo kama “Baba” au “Tinga”, pia alikuwa shabiki wa maisha yote wa klabu ya Gor Mahia FC, klabu yenye mafanikio makubwa zaidi nchini Kenya.
Siku chache kabla ya kifo chake, Oktoba 3, 2025, aliukaribisha uongozi wa Gor Mahia nyumbani kwake Karen na kuwapatia msaada wa Sh10 milioni 10 za Kenya kusaidia kampeni yao ya msimu wa 2025-2026.
Ujumbe wake wa mwisho kwa umma ulikuwa wa kuwatia moyo wachezaji na mashabiki wa timu hiyo akisema: “Nawatakia K’Ogalo kila la heri wanapopeperusha bendera ya kijani juu zaidi na kurejea tena kama mabingwa. Twende kazi Gor Mahia!”
Soka ilikuwa kama lugha ya kisiasa kwa Raila
Raila mara nyingi alitumia mifano ya soka kueleza hali za kisiasa, akilinganisha kushindwa kwa uchaguzi na kupoteza mechi, huku akifananisha ushindi na ubingwa.
“Siasa ni kama soka. Unaweza kutawala mchezo lakini bado ukapoteza. Lakini unaendelea kucheza mechi nyingine. Huhitaji kufunga kila mara; wakati mwingine, unachohitaji ni kudhibiti kiungo.”
Aliwahi kuelezea miungano ya kisiasa kama “mfumo wa uchezaji,” akieleza muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta kama mabadiliko ya mbinu za kuhakikisha nchi inapata utulivu kama kocha anavyobadilisha mfumo kutoka 4-4-2 hadi 3-5-2 ili kulinda uongozi.
Kupitia lugha ya soka, Raila aliweza kuungana na vijana wa Kenya, akitumia rejea za Arsenal “Invincibles” au mafanikio ya Gor Mahia katika michuano ya CAF, hivyo kufanya hotuba zake kuwa za kuvutia na zinazohusiana moja kwa moja na maisha ya mashabiki.
Aliwahi kusema kwa utani wakati wa kampeni: “Kama mashabiki wa Arsenal waliweza kuvumilia miaka 19 bila kombe, basi Wakenya wanaweza kuvumilia miaka mitano ya uongozi mbaya lakini tusiruhusu iwe kumi!”
Baada ya machafuko ya kisiasa ya 2007–08, Raila alianzisha mashindano ya soka katika mitaa ya mabanda ili kuhimiza upatanisho.
Alisema vijana wanapocheza pamoja, huacha kuona tofauti za kikabila na badala yake huona wenzao kama wachezaji wa timu moja.
Gor Mahia yampa heshima yake
Klabu ya Gor Mahia imetoa taarifa rasmi kupitia mitandao ya kijamii kuomboleza kifo cha mlezi wao mpendwa, Raila Odinga, ikimuelezea kama mwanga wa uongozi na nguzo ya klabu.
“Mioyo yetu imejaa huzuni tunapomlilia mlezi wetu mpendwa, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Alikuwa mwanga na nguzo muhimu kwa klabu yetu. Tunatoa pole kwa familia yake na wote walioguswa. Apumzike kwa amani kamilifu.”
Jumuiya nzima ya soka nchini Kenya imeungana kuomboleza kifo cha Raila Amolo Odinga, ikiomba roho yake ipumzike kwa amani.